• HABARI MPYA

    Wednesday, June 01, 2016

    TFF NA YANGA SASA 'NGUMI MKONONI' KISA UCHAGUZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MISIGANO imeibuka kuhusu uchaguzi wa Yanga SC ambayo sasa inawaacha njia panda wanachaa wa klabu hiyo, wakiwa hawajui washike lipi.
    Hiyo inafuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza na kuendesha mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo - wakati huo huo Yanga nayo ikitangaza na kuendesha mchakato yenyewe wa uchaguzi wake.
    Huku TFF ikiwa tayari imekwishaanza kutoa fomu za wagombea, Yanga nayo leo imeibuka na kutangaza zoezi zima la uchaguzi wake. 
    Katika mkutano wake na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit amesema ameagizwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu na Bodi ya Wadhamini kutangza tarehe rasmi ya uchaguzi tofauti na iliyotangazwa na TFF.
    Makao makuu ya Yanga, Jangwani, Dar es Salaam; Nani mwenye haki ya kuendesha uchaguzi kati ya klabu yenyewe na TFF?
    Baraka amesema hatua hiyo ya Yanga imefuatia kutokuwa na imani na TFF na kwamba hawako tayari kufanyiwa uchaguzi na shirikisho hilo.
    Baraka amesema uchaguzi wa Yanga utafanyika Juni 11 na si Juni 16 kama walivyosema TFF.
    Amesema fomu za wagombea zitaanza kutolewa Juni 2 hadi 3 na Juni 4 kitafanyika kikao cha mchujo wa awali wa wagombea na kuandika barua za kuwajulisha wagombea juu ya mchujo wa awali na kuchapisha na kubandika kwenye mbao za matangazo orodha  ya awali ya wagombea, zoezi ambalo litasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga na Sekretarieti.
    Juni 5 Kamati ya uchaguzi ya Yanga na Sekretarieti watapokea mapingamizi ya wagombea kama yatakuwapo na Juni 6 pingamizi zote zitapitiwa na kufanywa usaili wa awali, kabla ya kupeleka majina TFF yahakikiwe, kusikilizwa na kutolewa maamuzi ya masuala ya maadili.
    "Hiyo ni pamoja na kukata rufaa kwa maamuzi yaliotolewa, kusikilizwa rufaa na kutoa maamuzi ya rufaa na kisha kutangaza majina ya wagombea, zoezi ambalo sasa watafanya TFF na huo ndiyo utaratibu wa siku zote,"amesema Baraka.
    Baraka amesema Juni 7 hadi 10 wagombea watafanya kampeni zao kwa kujinadi kwenye matawi ya wanachama kabla ya Juni 11 kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Yanga, ukisimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu, chini ya uangalizi wa TFF.na Juni 12 matokeo yatatangazwa.
    Wakati Yanga wakitoa taarifa hizo kupitia kwa Kaimu Katibu wake, TFF nayo imetoa msistizo kwamba yenyewe ndiyo inaendesha mchakato wa uchaguzi wa Yanga.
    Taarifa ya Ofisa Habari wa TFF jioni ya leo, imesema kwamba mchakato wa uchaguzi wa Yanga unasimaiwa na Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho hilo kwa mujibu wa utaratibu walioutoa awali.
    Amesema fomu za uchaguzi zinaendelea kuchukuliwa katika ofisi za Makao Makuu ya TFF-Karume. Vilevile fomu zinaweza kupatikana kwenye tovuti ya TFF amayo ni www.tff.or.tz.
    "TFF inafuatilia kwa karibu mwenendo mzima wa mchakato na taarifa zote zitatolewa na TFF kupitia wasemaji wake na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ambaye ni Wakili Msomi, Alloyce Komba,".
    "Tayari Kamati ya Uchaguzi ya TFF, iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa Klabu ya Young Africans imeridhishwa na mwenendo wa wanachama kwa namna wanavyochukua na kurejesha fomu,".
    "Na kutokana na mipango yake, imesogeza mbele mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu mpaka Jumatatu Juni 6, 2016 saa 10:00 jioni," imesema taarifa ya TFF na kuendelea.
    "Hadi sasa wanachama tisa (9) wamechukua na kurejesha fomu. Wanachama hao ni Aaron Nyanda na Titus Osoro wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2010 inayotambulika serikalini hadi sasa,".
    "Wengine ni Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar. Uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Juni 25, 2016,".
    "Fomu zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Vilevile utaratibu unafanyika ili fomu ziweze kupatikana katika tovuti ya shirikisho www.tff.or.tz,"
    "Fomu zinapatikana kwa gharama ya Sh 200,000 kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti na Sh 100,000 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji," imemalizia taarifa ya TFF.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF NA YANGA SASA 'NGUMI MKONONI' KISA UCHAGUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top