Kikosi cha Yanga |
Na Mahmoud Zubeiry
MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
unakamilishwa leo kwa mechi moja kali kupigwa kwenye Uwanja wa Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga kati ya wenyeji Coastal Union na vinara wa ligi hiyo, Yanga SC.
Yanga imepania kushinda mechi hiyo ili kujiweka katika
mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu, ambayo mzunguko wake wa pili
utarejea Januari mwakani.
Wchezaji wa
Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts wamepania kuvunja rekodi ya
Coastal Union kutofungwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani, Mkwakwani, Tanga katika
mechi hiyo.
Nahodha
Msaidizi wa Yanga, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ alisema kwamba wanataka
kustawisha uongozi wao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuwafunga
Coastal Jumamosi.
Alisema wanajua
Coastal ni timu nzuri na wanatarajiwa upinzani katika mechi hiyo, ila ameonya
Yanga ya sasa ni tishio na wachezaji wako vizuri ‘ile mbaya’.
Lakini pia
habari za ndani kutoka Yanga zinasema kwamba tayari wachezaji wameahidiwa donge
nono iwapo watashinda mechi hiyo.
Wachezaji
hao, walizawadiwa Sh. Milioni 15 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC
mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Yanga
inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 26 na ikishinda dhidi ya Coastal itakwenda
kupumzika kwa raha sana.
Mkurugenzi
wa Ufundi wa Coastal, Nassor Bin Slum amesema Yanga watake wasitake watafungwa
Mkwakwani leo. Msimu uliopita, Yanga waliifunga Coastal mechi zote, kwanza 5-0
Dar es Salaam na 1-0 Tanga.
Lakini
Coastal ya mwaka huu ni nyingine kabisa, kwani imesajili wachezaji wazuri na
wazoefu. Nsa Job hatakuwapo kwa sababu anaumwa goti, lakini yupo mkali mwingine
wa mabao katika timu hiyo, Daniel Lyanga.
Burudani
zaidi inatarajiwa kuwa katika safu ya kiungo, Coastal kuna Razack Khalfan na
Jerry Santos na Yanga wapo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Haruna Niyonzima. Yanga
wameshinda mechi mbili za ugenini kati ya tano, wametoa sare moja, wamefungwa
mbili pia.
Katika mechi za jana, bao pekee la Mussa Said Kimbu dakika ya
73, leo liliizamisha Simba SC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kimbu alifunga bao hilo akiunganisha krosi ya Mganda, Mohamed
Jingo tena akipitisha mpira katikati ya msitu wa mabeki wa Simba na kipa wao,
Wilbert Mweta.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo, Azam ilifungwa 2-1 na
Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Lyon ikafungwa 3-1 na Mtibwa
Sugar, Kagera Sugar ikatoka sare ya bila kufungana na Polisi Morogoro, JKT Oljoro
ikafungwa 3-1 na Ruvu Shooting na Prisons ikatoka sare ya 1-1 na JKT Ruvu.