• HABARI MPYA

    Sunday, November 11, 2012

    MASWALI MENGI BILA MAJIBU SAKATA LA RUSHWA AZAM


    SOKA ya Tanzania imechafuka tena kwa tuhuma chafu za hongo katika mchezo, ambazo zimewaponza wachezaji wanne wa klabu ya Ligi Kuu, Azam FC, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kupoteza ajira zao.
    Na Mahmoud Zubeiry

    Nasema kupoteza ajira zao, kwa sababu baada ya kuwasimamisha, viongozi wa Azam wamesema hawawahitaji tena wachezaji hao katika timu yao na mwakani watakisuka upya kikosi chao.
    Nani atasajili wachezaji wauza mechi kati ya timu kubwa za Tanzania, ina maana hao ndio mustakabali wao kisoka umeharibika.
    Dida, Nyoni na Morris wote hawa ni wachezaji wa Taifa Stars, tena tangu enzi za Mbrazil Marcio Maximo tazama hasara tunayoelekea kuipata na inauma zaidi kwa nafasi ya beki ya kati, ambayo wachezaji wake wamekuwa adimu nchi hii kwa miaka ya karibuni.
    Bado najiuliza, ni kweli wachezaji hawa walihujumu timu yao, ama ni dhana tu au wamefitiniwa?
    Soka ya nchi hii inakwamishwa na mambo mengi sana, lakini kubwa ni uelewa mdogo wa wengi kati ya viongozi wetu, ambao wanaingilika kwa urahisi mno kimajungu na fitina. Nina wasiwasi kwamba inawezekana wachezaji hawa wamefitiniwa, lakini pia siwezi kubisha juu ya tuhuma hizi kwa sababu haya mambo yapo.
    Kumbuka, Azam ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi za Ligi Kuu na baada ya hapo ikamfukuza kocha wake Mserbia, Boris Bunjak na kumrejesha Muingereza, Stewart Hall.
    Bunjak alifukuzwa kwa sababu ya kushuka kwa uwezo kwa timu kwa kipindi alichokuwa kazini, kwa mujibu wa Azam wenyewe, lakini kumbe wachezaji walikuwa wanamsaliti kwa mujibu wa Azam pia.
    Ndiyo, alifungwa mechi moja tu kwenye Ligi Kuu, hiyo ya 3-1 na Simba na baada ya hapo akafukuzwa, baadaye inakuja kujulikana wachezaji walipewa fedha wahujumu timu. Tazama mkanganyiko huu.
    Habari kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata taarifa hizo, uongozi ulizifanyia kazi kwa kushirikisha hadi na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo ilipokamilisha uchunguzi wake wakatoa ripoti inayowataja wachezaji hao wanne kupokea rushwa kutoka kwa kiongozi mmoja wa Simba.
    Wachezaji tumewajua, tumewajua kutokana na taarifa za wenyewe Azam, lakini huyu kiongozi ni nani na kwa nini naye asitajwe?
    Azam inadhani imewatendea haki kuwatangaza wachezaji hawa kuhusika na tuhuma hii nzito, bila ya kumtaja mtuhumiwa mwingine, ambaye haswa ndiye kirusi, huyo aliyewahonga?
    Bado nakumbuka Dida hakucheza mechi hiyo, kwani Oktoba 27, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim, Himid Mao aliyempisha Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Herman Tcheche na Salum Abubakar.
    Siku hiyo, Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
    Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka mabeki wa Azam.
    Hivyo basi, Dida hata kama alipokea hongo aliitumikiaje na si yeye aliyesimama langoni?
    Hapo hapo, tunaambiwa TAKUKURU imefanyia kazi suala hilo, tunafahamu kwa mujibu wa sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania rushwa ni kosa la jinai, na je nini kinachofuata sasa baada ya kuwatia hatiani wachezaji na huyo kiongozi wa Simba?
    Huku kwetu kwenye mpira rushwa haitakiwi kabisa na kushiriki au kuhusika kwa namna yoyote katika kashfa hiyo ni ukosefu wa uadilifu na soka haihitaji kiongozi wala mchezaji asiye mwadilifu.
    Pamoja na hayo, kwa muda mrefu tu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeendelea kukaa kimya kabisa.
    Nakumbuka sakata la Shaaban Kado na Ulimboka Mwakingwe Morogoro mwaka juzi na bado kuna mambo mengi tu mengine tu yanazungumzwa, lakini TFF ipo kimya kana kwamba nayo inasapoti mchezo mchafu katika soka yetu.
    Wakati mwingine maneno yanazungumzwa kwamba kuna baadhi ya klabu zinahonga hadi maofisa wa TFF ili wawekewe mambo fulani fulani kwa matakwa yao, mfano kupangiwa marefa wanaowataka na aina ya ratiba wanayotaka wao.
    Soka yetu imechafuka kwa kweli. Tukirejea kwenye sakata la Azam, klabu hiyo izingatie ina mikataba na wachezaji hao na iliwasajili kwa fedha na bila shaka walikuwa kwenye mipango yao ya muda mrefu.
    Je, kuwafukuza tu ni dawa na pia ni kuwatendea haki? Bado sioni kama tunakaribia hata robo ya suluhisho la tatizo hili.
    Hapo juu nimesema, Bunjak alifukuzwa kwa sababu ya madai ya kushuka kwa kiwango cha timu, lakini kumbe wachezaji walimhujumu! Na hapa klabu imepata hasara kwa kuvunja mkataba na kocha na kumlipa fedha nyingi, kisha kuajiri kocha mwingine.
    Maana yake, hasara hii imeletwa na hawa wachezaji walioufanya uongozi uamini Bunjak si kocha mzuri. Tazama jinsi ambavyo sakata hili linavyozalisha maswali mengi yasiyo na majibu.  Hiyo ndio soka ya bongoi!
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MASWALI MENGI BILA MAJIBU SAKATA LA RUSHWA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top