African Lyon |
Na Mahmoud Zubeiry
MARIO Balotelli sifa yake kubwa ni utukutu na kadi kibao
uwanjani- basi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ukiwasaka wachezaji
wenye sifa kama za Mtaliano huyo mwenye asili ya Ghana anayechezea Manchester
City unaweza kuwapata kwa urahisi katika klabu ya African Lyon ya Dar es
Salaam.
Hadi sasa, ikiwa imecheza mechi 11 za Ligi Kuu, Lyon
inaongoza kwa adhabu za kadi, ikiwa ina kadi 30, kati hizo mbili ni nyekundu na
28 za njano.
Mtibwa Sugar inafuatia kwa kuwa na watukutu wengi kikosini,
hadi sasa ikiwa na kadi 22, kati ya hizo mbili ni nyekundu.
Mgambo ndio inafuata kwa kuwa na akina Balotelli wengi, hadi
sasa ikiwa imepewa kadi 23, ingawa bahati nzuri kwao zote ni za njano, wakati
Toto African ni ya tatu kwa kucheza mchezo usio wa kiungwana, ikiwa ina kadi
22, kati ya hizo moja nyekundu.
JKT Oljoro nayo pia ni pango la watukutu, kwani hadi sasa ina
kadi 21 na kati ya hizo mbili nyekundu, Azam nayo si haba akina Balotelli wapo
wapo, kwani hadi sasa katika mechi 10 ilizocheza imevuna kadi 16, moja
nyekundu, sawa kabisa na Coastal Union na Polisi Morogoro.
Prisons, Ruvu Shooting na JKT Ruvu, zote zina kadi 16 za
njano tupu kila mmoja, wakati kwa wapinzani wa jadi, Yanga wanawazidi Simba kwa
mchezo wa kiungwana, hadi sasa wana kadi 10 za njano na moja nyekundu, wakati
mahasimu wao wana kadi 13 za njano na mbili nyekundu. Kagera Sugar wana kadi 14m,
zote za njano.
P Y R T
AFRICAN LYON 11 28 2 30
MGAMBO JKT 10 23 0 23
MTIBWA SUGAR 10 20 2 22
TOTO AFRICAN 11 21 1 22
JKT OLJORO FC 11 19 2 21
COASTAL UNION 11 14 2 16
POLISI 11 15 1 16
AZAM FC 10 15 1 16
PRISONS FC 9 16 0 16
RUVU SHOOTING 10 16 0 16
JKT RUVU SC 10 16 0 16
SIMBA SC 11 13 2 15
KAGERA SUGAR 11 14 0 14
YANGA SC 11 10 1 11
(P idadi ya mechi ilizocheza, Y njano, R nyekundu na T ni
jumla)