• HABARI MPYA

    Tuesday, August 21, 2012

    MTAKATIFU TOM ASIKITISHWA NA POULSEN, TFF KUMREJESHEA SPIDER MAN MAJERUHI BILA TAARIFA

    Mtakatifu Tom kushoto, akiwa na BIN ZUBEIRY 

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba mshambuliaji wake Said Bahanuzi ‘Spider Man’ aliumia goti akiwa na timu ya soka taifa ya Tanzania, Taifa Stars, lakini anasikitika si kocha wa timu hiyo, Mdenmark, Kim Poulsen wala kiongozi yeyote wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), aliyeipa taarifa klabu hiyo juu ya tatizo la mchezaji huyo.
    Bahanuzi 'Sp;ider Man'
    Mtakatifu Tom amesema kwamba anasikitishwa mno na hilo, kwani ni kinyume cha utaratibu. “TFF walipaswa kusema baada ya mchezaji kurudi klabuni kwamba ana matatizo haya, lakini hawajasema kitu hadi leo, imenisikitisha sana,”alisema Tom.    
    Yanga jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya African Lyon bila kinara wake huyo wa mabao  na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga ilitumia mchezo huo kuwapima wachezaji wake kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu na haukuwa mwanzo mbaya, timu ikicheza kwa utulivu na hata kuhimili vishindo vya wapinzani.
    Didier Kavumbangu, mshambuliaji mpya wa klabu hiyo aliyesajiliwa kutoka Atletico Olympique ya Burundi, alikuwa wa kwanza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya sita baada ya kupiga mpira uliombabatiza beki wa Lyon na badaye kumgonga kipa na kuingia nyavuni.
    Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0 na kipindi cha pili, Haruna Niyonzima aliifungia Yanga bao la pili kwa penalti dakika ya 57, baada ya Simon Msuva kuchezewa rafu na Semmy Kessy kwenye eneo la hatari.
    Frank Damayo aliyeingia kuchukua nafasi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ kipindi cha pili alitoa pasi nzuri kwa Simon Msuva ambaye aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 72, kabla ya Jerry Tegete kufunga la nne dakika ya 90+1.  
    Baada ya mchezo huu, Yanga ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam leo sa 10:00 jioni kwenda Kigali, Rwanda ambako itaweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na Ligi Kuu.
    Ikiwa huko, Yanga itacheza mechi kadhaa za kujipima nguvu na vigogo wa Rwanda, kama APR, Rayon, Atracao na Polisi kabla ya kurejea Dar ves Salaam kuanza maandalizi ya Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTAKATIFU TOM ASIKITISHWA NA POULSEN, TFF KUMREJESHEA SPIDER MAN MAJERUHI BILA TAARIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top