• HABARI MPYA

    Sunday, June 10, 2012

    TAIFA STARS KUMALIZA GUNDU LA TAIFA LEO?


    Samatta anayetarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji Stars leo
    hapa akidhibitiwa na kolo Toure Jumamosi iliyopita Abidjan

    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo inashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Gambia katika mechi ya pili ya Kundi C, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.
    Stars ambayo mechi ya kwanza ilifungwa 2-0 na wenyeji Ivory Coast mjini Abidjan Jumamosi iliyopita, itacheza mechi ya tatu chini ya kocha mpya, Kim Poulsen, aliyerithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
    Poulsen amekiri kucheza mechi mbili bila kufunga hata bao moja, sare ya bila kufungana na Malawi na kichapo cha 2-0 cha Ivory Coast, lakini amesema timu yake imebadilika mno na anatarajia mabao katika mchezo wa leo.
    Poulsen amesikitishwa na kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kushindwa kumpatia DVD za mechi za Gambia kuelekea mechi ya leo na jana alisema hiyo ni mara ya pili anaomba DVD, lakini anashindwa kupatiwa, baada ya awali kuomba DVD za Ivory Coast.
    Pamoja na kukosa DVD hizo, lakini Poulsen amesema amewaandaa vizuri vijana wake kwa ajili ya mechi hiyo, ili washinde na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania tiketi ya Brazil 2014.
    Poulsen alisema kambi yake iko vizuri na anafurahi kiungo mshambuliaji Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ aliyekuwa mgonjwa kiasi cha kukosa safari ya Ivory Coast, anaendelea vizuri na anaweza akaanza leo.
    Kwa upande wake, kocha wa Gambia, Mtaliano, Luciano Machini amesema mechi ya leo itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao ni wazuri.
    Machini aliyechukua nafasi ya aliyekuwa bosi wake, Peter Bonu Johnson, Mei mwaka huu, amesema kwamba Taifa Stars ni wazuri na wana kasi uwanjani, hivyo mechi hiyo hata wachezaji wake wanajua itakuwa ngumu.
    Alisema wao walicheza vizuri dhidi ya Morocco kwenye mechi yao ya kwanza, lakini wanaingia kwenye mechi ngumu na wenyeji leo.
    Nge wa Gambia waliotoka sare ya 1-1 nyumbani na Morocco kwenye mechi ya kwanza Jumamosi, wamecheza mechi nne bila kushinda, tangu washinde kwa mara ya mwisho Agosti 10, mwaka jana mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Ilifungwa 1-0 na Namibia Septemba 3, mwaka jana, ikatoka sare ya 1-1 na Burkina Faso Oktoba 8, mwaka jana, ikafungwa 2-1 na Algeria Februari 29, mwaka huu kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Morocco nyumbani Jumamosi iliyopita.
    Rekodi ya Tanzania pia si nzuri katika mechi za nyumbani na tangu iifunge Jamhuri ya Afrika ya Kati Machi 26, mwaka jana haijashinda tena mechi kwenye Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 na imecheza saba baada ya hapo.
    Katika mchezo wa leo, kikosi cha Stars kinatarajiwa kuwa; J. Kaseja, Kelvin Yondan, Amir Maftah, Juma Nyosso, K. Yondan, M. Ngassa, S. Nditi, M. Kazimoto, M. Samata, H. Moshi na S. Abubakar.
    Gambia: C. Allen, A. Jammeh, O. Koli, M. Danso, T. Jaiteh, Y. Ceesay, P. Jagne,   
    P. Kujabi, M. Jarju D. Savage na M. Ceesay.
    Kikosi cha Stars kilichoifunga Afrika ya Kati

    MATOKEO YA STARS TAIFA TANGU ISHINDE MARA YA MWISHO:
    Machi 26, 2011:     Tanzania    2 – 1    Afrika ya Kati  (Kufuzu CAN)
    Mei 14, 2011:         Tanzania    0 – 1    Afrika Kusini   (Kirafiki)
    Sept 3, 2011:          Tanzania   1 – 1    Algeria            (Kufuzu CAN)
    Nov 15, 2011:        Tanzania     0 – 1     Chad                (Kufuzu Kombe la Dunia)  
    Des 3, 2011:            Tanzania  1 – 2   Zimbabwe     (Kirafiki)
    Feb 23, 2012:         Tanzania   0 – 0   DRC                (Kirafiki)    
    Feb 29, 2012:         Tanzania   1 – 1   Msumbiji         (Kufuzu CAN) 
    Mei 26, 2012:         Tanzania   0 – 0   Malawi             (Kirafiki)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS KUMALIZA GUNDU LA TAIFA LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top