• HABARI MPYA

    Thursday, June 07, 2012

    SAKATA LA YONDAN; YANGA WAMPA RAGE DAWA YA KUTULIZA MAUMIVU

    Yondan akisaini risiti za kupokea malipo yake Yanga jana
    KLABU ya Yanga imetoa ufafanuzi kuhusu usajili wa beki Kelvin Patrick Yondan, kwamba jana hakuwa anasaini fomu za mkataba, bali risiti za malipo ya fedha zake, baada ya kuwa amekwishasani tangu alipomaliza mkataba wake Simba SC.
    Abdallah Ahmad Bin Kleb aliyefanikisha usajili huo kwa pamoja na Seif Ahamd 'Magari' wameiambia BIN ZUBEIRY usiku huu kwamba, Yondan alikuwa anadai Sh. Milioni 15, baada ya awali kupewa Sh. Milioni 15 na kwa hofu ya labda asingemaliziwa fedha zake, akakana kusaini Yanga.
    Lakini, maswahiba hao wawili wamesema baada ya kummalizia fedha zake Yondan jana, mambo safi na amewathibitishia kwa viapo vyote kwamba hajasaini Simba na yuko tayari kufika popote kwenye vyombo vya sheria dhidi ya mwajiri wake wa zamani, kutetea haki zake.
    Yondan mwenyewe jana aliihakikishia BIN ZUBEIRY kwamba hajasaini Simba na yeye ni mchezaji halali wa Yanga.
    Lakini leo, Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage aliitisha Mkutano na Waandishi wa Habari, akisema atawashitaki Yanga FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kwa kitendo cha kumsajili mchezaji wao kinyume cha kanuni na sheria za usajili.
    Rage, Mbunge wa Tabora mjini (CCM), alidai Simba ilikwishaongeza mkataba na Yondan kabla hajasaini Yanga na akaonyesha nakala za mikataba, ingawa saini za mikataba inayoonyeshwa na klabu zote, zinatofautiana.    
    Kwa Simba, hili ni pigo la tatu wanapata kutoka kwa watani wao, awali walitangaza kumsajili kiungo Nizar Khalfan, lakini baadaye mchezaji huyo akaibukia Yanga. Aidha, Rage alikaririwa akitamba hakuna mchezaji yeyote wa Simba anayeweza kwenda Yanga, ila sasa Barthez na Yondan 'wanamuumbua' mtu mzima huyo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAKATA LA YONDAN; YANGA WAMPA RAGE DAWA YA KUTULIZA MAUMIVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top