![]() |
| Maximo akiwa na Kikwete |
Na Anna Nkinda - Sao Paul, Brazil
ALIYEWAHI kuwa kocha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa
Stars, Mbrazil Marcio Maximo amesema hana ndoto za kurejea kufundisha soka
Tanazania tena.Sambamba na hilo, Maximo amezishauri klabu za Tanzania, ili kuwa na timu nzuri zinapaswa kuwekeza kuanzia ngazi ya watoto wenye umri wa miaka nane, vijana na kuendelea ili kupata timu bora ya Taifa.
Maximo alisema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Sao Paul, Brazil.
Maximo alisema kuwa timu nyingi ambazo ni bora na zinafanya vizuri katika mchezo wa soka zimekuwa zikiwaandaa watoto wenye vipaji vya mchezo huo wangali wadogo ili waweze kuwa wachezaji wazuri hapo baadaye.
Kuhusiana na uvumi ulioenea kuwa anataka kwenda kufundisha timu za Taifa Stars, Azam na Yanga alisema kuwa siyo kweli na wala hajawasiliana na timu hizo na hawezi kwenda kufundisha kwani hivi sasa anamkataba wa kufundisha timu ya Democrata iliyopo nchini humo.
“Timu ya Taifa Star inakocha mzuri, ambaye ninamuheshimu na ninaukubali ufundishaji wake hivyo basi kupitia kocha huyo ninaamini watanzania watazidi kuendelea katika soka na kufika mbali zaidi”, alisema.
Maximo alimalizia kwa kusema kuwa ana mawasiliano mazuri na watanzania na anawapenda ndiyo maana kila mahali anapopita anajivuna na kusema kuwa Tanzania ni nchi yake ya pili.
Hivi sasa Maximo ni kocha wa timu ya Democrata iliyopo nchini humo ambapo wiki ijayo inatarajia kuanza mashindano ya taifa yatakayopelekea kupata wachezaji bora watakaoshiriki mashindano ya kombe la Dunia yanayotarajia kufanyika mwaka 2014 nchini Brazil.
Watanzania wanamkumbuka sana Maximo kwa jitihada zake za kukusa soka katika nchi hii alipokuwa akifanya kazi kati ya mwaka 2006 hadi 2010 makataba wake ulipoisha akaondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Mdenmark, Jan Borge Poulsen ambaye chini yake soka ya nchi imedoda.
Aliifanya Tanzania kuwa mshindani wa kweli kwenye michuano ya kimataifa na mwaka 2008 iliikosakosa kidogo tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, ilipofungwa na Msumbiji katika mechi ya mwisho nyumbani.
Mwaka 2009 aliiwezesha Taifa Stars kucheza fainali za kwanza za michuano ya CHAN nchini Ivory Coast, inayohusisha wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee.
Tanzania ilikaribia kuingia Nusu Fainali kama si kushindwa kulinda bao dhidi ya Zambia na kufungwa bao la dakika za lala salama na kupata sare ya 1-1 hivyo kutolewa katika Kundi A.
Maximo pia atakumbukwa kwa kuiwezesha Tanzania kucheza mechi ya kirafiki na kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Brazil, kiliochokuja na nyota wake wote kabla ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.



.png)
0 comments:
Post a Comment