• HABARI MPYA

    Sunday, August 14, 2016

    SIMBA SC YABANWA NA URA, SARE 1-1 TAIFA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imebanwa na URA ya Uganda baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
    Mabao yote yalipatikana kipindi cha kwanza katika mchezo huo wa mwisho wa kujipima nguvu kwa timu ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wiki ijayo.
    Aliyekuwa nahodha wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi alicheza kwa dakika tatu kabla ya kukamata mpira na kuubusu kisha kuwapungia mkono mashabiki kuwaaga akiashiria kustaafu rasmi soka kwa ujumla.
    Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude (kushoto) akikimbia kushangilia baada ya kufunga leo
    Nafasi ya Mgosi aliyekwenda kuzunguka pembeni za mwa jukwaa na mtoto wake mdogo kuaga, ilichukuliwa na kiungo mpya, Jamal Mnyate aliyesajiliwa kutoka Mwadui FC ya Shinyanga.
    Mgosi aliyepokewa na familia yake, ikiongoawa na mkewe Jasmine baada ya kutoka uwanjani – sasa anakuwa Meneja wa Simba SC.
    URA walitangulia kwa bao Shafiq Kagimu aliyefumua shuti dakika ya 19 baada ya kupokea krosi ya Labama Bokota.
    Simba ilikuja juu mara baada ya bao hilo na dakika ya 26 Mrundi Laudit Mavugo na Mnyate walishindwa kuunganisha krosi nzuri ya beki wa kushoto Hamad Juma mpira ukaokolewa na mabeki.
    Simba ikafanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 32 kupitia kwa Nahodha mpya, Jonad Gerald Mkude aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na beki wa kushoto, Mohemed Hussein ‘Tshabalala’ kufuatia Hamad Juma kuchezewa rafu.
    Beki wa kulia wa Simba, Hamad Juma akimtoka beki wa URA
    Winga wa Simba, Shizza Kichuya akipasua katikati ya wachezaji wa URA 

    Nahodha wa zamani na Meneja mpya wa Simba, Mussa Hassan Mgosi alicheza kwa dakika tatu, lakini mabeki wa URA waliikubali shughuli yake

    Baada ya bao hilo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kosa kosa za mabao zikawa za pande zote hadi mwisho wa mchezo.
    Mchezaji ghali zaidi kwenye kikosi cha sasa cha Simba, mshambuliaji Muivory Coast, Frederick Blagnon aliingia kumpokea Ibrahim Hajib kipindi cha pili, lakini kwa mara ya pili akashindwa kuwafurahisha mashabiki Uwanja wa Taifa.
    Mchezaji huyo aliyesajiliwa kwa dau la zaidi ya Sh. Milioni 100, alipiga shuti moja tu dhaifu kwenye lango la URA baada ya kuingia dakika ya 79.  
    Safu ya kiungo ya Simba SC leo haikucheza vizuri kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita wakishinda 4-0 dhidi ya AFC Leopard ya Kenya na haikuwa ajabu leo Hajib hakufunga, kwa sababu muda mwingi alilazimika kutafuta mpira kuliko nafasi za kufunga. 
    Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Vincent Angban, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hamad Juma, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya/Hajji Ugando dk74, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Hajib/Frederick Blagnon dk79 na Mussa Mgosi/Jamal Mnyate dk3/Mussa Ndusha dk62.
    URA FC; Oscar Agaba, Mathias Muwanga, Sam Sekito, Fahad Kawoya, Shafiq Kagimu, Jimmy Lule, Feni Ali, Labama Bokota, Julius Ntambi na Elkanah Nkugwa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YABANWA NA URA, SARE 1-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top