• HABARI MPYA

    Sunday, June 12, 2016

    SIMBA SC WAKIFANYIA KAZI USHAURI WA KAPUYA MAMBO YATANYOOKA

    MOJA kati ya timu zilizokuwa tishio katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara miaka ya 1980 na 1990 ni Pamba ya Mwanza, ambayo kwa bahati mbaya sasa inasota madaraja ya chini.
    Pamba ilikuwa maarufu kwa kuibua nyota wengi waliogeuka tishio katika soka ya Tanzania – lakini ilikuwa inaongoza kuchukuliwa wachezaji wake na timu kubwa, Simba na Yanga.
    Pamba ikaitwa Chuo cha Kuzalisha wanasoka nyota nchini, kwa sababu tu kila baada ya msimu wachezaji wake wengi walichukuliwa Simba na Yanga, lakini msimu mpya ilikuwa inaibuka na wachezaji wengine ambao waliendelea kuzitamanisha timu kubwa.
    Na haikuwahi kutokea eti Pamba ikatunishiana msuli na ama Simba au Yanga kugombea mchezaji wa timu yoyote, bali iliwaacha waliotaka kuondoka na msimu mpya ikawa inaibua wakali wengine.

    Bahati mbaya sana, Pamba ikapotea mwishoni mwa milenia iliyopita na si kwa sababu yoyote zaidi ya kutemwa na Bodi ya Pamba waliokuwa wamiliki.
    Mkoa wa Mwanza ukajaribu kuichukua timu kuiendeleza baada ya kutemwa na Bodi, lakini ikashindwa na timu ikapoteza makali hadi kupotea kwenye ramani ya soka nchini.
    Nini ilikuwa siri ya mafanikio ya Pamba wakati huo? Ilitumia zaidi eneo dogo tu la Kanda ya ziwa kujipatia wachezaji chipukizi wazuri kila msimu tena kwa bajeti ndogo tu.
    Kwa miaka minne, sasa Simba SC imeyumba na kuziachia utawala wa soka ya nchi Azam na Yanga.
    Na Rais wa Simba SC, Evans Aveva katika taarifa yake ya kufunga msimu uliopita moja ya sababu alizotaja ni ya timu kuzidiwa kifedha na Azam na Yanga.
    Lakini pia, Aveva akasema hizi ni zama nyingine kabisa ambazo Ligi Kuu ina wadhamini wawili ambao wanagawa fedha kwa timu zote za ligi hiyo, hivyo kuzifanya ziwe imara na kuongeza ushindani.
    Na kwa sasa wakati zoezi la usajili linaendelea, inaonekana wazi Simba inazidiwa kete na Azam na Yanga katika kuwapata wachezaji wazuri.       
    Kitu hicho amekiona hata Waziri wa zamani wa Michezo Tanzania, Profesa Juma Athumani Kapuya na amewashauri Simba waache kushindana na Azam na Yanga katika usajili.
    Kapuya amesema kwamba ni kweli kwa sasa Simba inazidiwa uwezo kiuchumi na Azam na Yanga, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kutopata wachezaji wazuri wa kusajili.
    “Kwanza nataka niwashauri jambo moja Simba, waache kushindana na Azam na Yanga. Wakati huu ambao Azam na Yanga wanasajili, wao watulie tu. Wawaache Azam na Yanga wasajili, naamini Azam na Yanga hawawezi kuwafikia wachezaji wote wazuri. Sasa wale watakaobaki ndiyo watakuja Simba kiulaini,”alishauri Kapuya ambaye ni mpenzi wa Simba.
    Pamoja na hayo, Kapuya alisema hafurahishwi na tabia ya sasa ya Simba kusajili wachezaji chipukizi na kuwauza wanapokomaa, kipindi ambacho ndiyo wanatakiwa waanze kuisaidia timu.
    Ametoa mfano wachezaji waliosajiliwa wakiwa chipukizi kama beki Shomary Kapombe na kiungo Ramadhani Singano ‘Messi’ wote waliuzwa katika kipindi ambacho michango yao ilitakiwa kuanza kuonekana Simba.
    “Namna hiyo kila siku utakuwa unaanza upya. Lazima uongozi wa Simba uwe na uchungu na timu, uhakikishe wachezaji hawaondoki kwa urahisi. Lakini pia kuna suala la kuishi nao vijana ili wakati wote wafurahie kuwapo Simba, nalo viongozi wa Simba walitazame, wasijiruhusu kugombana gombana na wachezaji, na wahakikishe wanawatimizia ahadi, hapo wataishi nao vizuri,”alisema Kapuya.
    Waziri huyo amesikitishwa pia na desturi ya viongozi wa Simba kufukuza wachezaji wazuri kama ilivyowahi kutokea kwa viungo Amri Kiemba, Haroun Chanongo na washambulaji Elias Maguri na Amissi Tambwe na akawataka pia kuwa makini kutosajili wachezaji wenye mapenzi na mahasimu wao, kama Hassan Kessy.
    “Pia wawachunguze wachezaji kabla ya kuwasajili, ili wasije kurudia kusajili akina Kessy wengine hapa, lazima mchezaji ujue huko alipotokea alikuwa ana desturi zipi, ukitaka kujua utajua. Lakini ukikurupuka kumsajili bila kujua, ndiyo hivyo,”amesema Kapuya.
    Ninaona kabisa ushauri wa Kapuya ni mzuri kwa Simba, kwamba katika kipindi hiki wanapaswa kutulia na kuwasoma wapinzani wao, Azam na Yanga, kabla ya kuanza kusajili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAKIFANYIA KAZI USHAURI WA KAPUYA MAMBO YATANYOOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top