• HABARI MPYA

    Wednesday, June 08, 2016

    BILA SHAKA, HII NDIYO MAANA YA USAJILI HUU WA YANGA

    JUZI klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, imesajili wachezaji wengine wapya wawili, ambao ni kipa Benno Kakolanya kutoka Prisons ya Mbeya na beki Andrew Vincent ‘Dante’ kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.
    Usajili wa wawili hao, unafanya idadi ya jumla ya wachezaji wapya waliosajiliwa Yanga SC kufika wanne, baada ya beki Hassan Kessy kutoka Simba SC na kiungo Juma Mahadhi kutoka Coastal Union.
    Wachezaji wote wapya waliosajiliwa Yanga hadi sasa ni vijana wadogo walio chini ya umri wa miaka 23, ambao unaweza kusema kama watapata malezi mazuri wataisaidia klabu baadaye.

    Kwa sasa, kikosi cha Yanga kimesheheni vizuri tu kila idara ikiwa na mchezaji zaidi ya mmoja aliye katika kiwango cha kimataifa, kitu ambacho ni wastani mzuri katika timu.
    Lakini ukitazama aina ya wachezaji waliopo Yanga kwa sasa wengi wao ni ambao baada ya miaka miwili kuanzia sasa uwezo wao unaweza kuanza kushuka kutokana na umri na kutumika kwa muda mrefu.
    Maana yake, Yanga inahitaji kuanza kuingiza vijana wapya wa kuanza taratibu kuandaliwa kwa ajili ya kuja kuchukua nafasi baadaye.  
    Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu tunashuhudia aina fulani ya usajili rahisi kuuelewa dhamira yake tofauti na tulivyozoea kuona usajili wa sifa na mwembwe. 
    Andrew Vincent ni kijana mdogo ambaye misimu miwili ijayo anaweza kuanza kucheza katika eneo lenye wakongwe watupu Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mtogo Vincent Bossou.
    Pato Ngonyani ni chipukizi mwingine, beki wa kati ambaye tayari yupo kikosini Yanga, anaendelea kutayarishwa kuwa beki tegemeo wa timu baadaye.
    Nafasi za mabeki wa kati ni shida dunia nzima na klabu nyingi huyumba baada ta kupoteza wachezaji wao wa nafasi hizo.
    Lakini kama kunakuwa na mipango ya muda mrefu ya aina hii, unaweza kuepukana na matatizo ya aina hiyo.
    Hata Cannavaro ambaye amefikisha miaka 10 tangu ajiunge na Yanga, alisajiliwa mwaka 2006 na misimu miwili ya mwanzoni alilazimika kuwatazama Lulanga Mapunda na Hamisi Yussuf wakianzishwa pamoja.   
    Beki wa kulia wa Yanga ni Juma Abdul ambaye huwezi kumuweka katika kundi la wachezaji vijana wadogo tena – kuingia kwa Kessy wazi ni mtu ambaye atachukua nafasi hiyo baadaye.
    Kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ anaelekea ukingoni na Deo Munishi ‘Dida’ naye si kipa mdogo tena, wakati Benedicto Tinocco ameshindwa kumudu ushindani wa nafasi baada ya misimu miwili ya kuwapo Yanga.
    Unaona kabisa kuingia kwa Kakolanya ni mpango mwafaka na katika wakati mwafaka, iwapo tu kipa huyo chipukizi atakwenda Yanga kwa dhamira ya siku moja awe kipa tegemeo wa timu.
    Ukiondoa viungo wa kikosi cha kwanza, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Yanga ina viungo wengine wawili wazawa ambao ni Said Juma ‘Makapu’ na Salum Telela.
    Wote ni wachezaji wazuri, lakini kuongezeka kwa Mahadhi kijana mdogo mno chini ya umri wa miaka 20 ni kuimarisha safu hiyo na kuwapa changamoto Makapu na Telela wasilale.
    Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm amesajili vijana wadogo ambao kama wanaweza kwenda kuwa na subira, baadaye watakuwa magwiji wa klabu.
    Mfano mdogo, msimu uliopita Yanga ilisajili vijana wadogo wawili wa safu ya ushambuliaji, Malimi Busungu na Matheo Anthony, ambao waliridhika kupewa muda mchache wa kucheza mbele ya Mzimbabwe Donald Ngoma na Mrundi Amissi Tambwe kwa matarajio yaliyomo vifuani mwao.
    Pamoja na nafasi chache walizopata kila mmoja alionyesha umuhimu wake katika timu kwa kufunga mabao katika mechi muhimu.
    Lakini Desemba mwaka jana, Yanga ikamsajili mtu mzima Paul Nonga, ambaye baada ya miezi sita anaomba kuuzwa kuliko kundelea kuwa mchezaji wa mechi nyepesi.
    Nonga ni mchezaji ambaye anahesabu miaka kuelekea mwisho wake wa kucheza soka ya ushindani – hivyo anahitaji kutumia kipindi hicho vizuri na si ajabu anataka kuondoka Yanga ambako analipwa vizuri kwa sababu anaona kuna sehemu nyingine labda atalipwa vizuri na kucheza pia.
    Yanga imefanya usajili mzuri wa malengo, vijana wapya waliosajiliwa tu wasiwe na papara, wasilewe sifa, wasibweteke – waende kufanya bidii, wawe na subira, nidhamu na kujituma hawajakosea kusaini Jangwani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BILA SHAKA, HII NDIYO MAANA YA USAJILI HUU WA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top