• HABARI MPYA

    Thursday, November 08, 2012

    SOKA YETU INAELEKEA WAPI?

    Wachezaji wa Simba na Azam

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA SC hawajawasimamisha kipa wao Mghana, Yaw Berko na beki Stefano Mwasyika, ila wameamua kutowatumia wakiamini wanawahujumu wakitumiwa na Simba na Azam.
    Simba wamewasimamisha Juma Nyosso na Haruna Moshi, wakiamini wanatumiwa na Yanga na Azam kuihujumu timu yao.
    Na leo, Azam wamewasimamisha Deo Munishi ‘Dida’, Said Mourad na Erasto Nyoni wakiamini wanatumiwa na Simba na Yanga kuihujumu timu hiyo.
    Hizi ni klabu tatu ambazo zinachuana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kwa sasa ndizo zinaibeba soka ya Tanzania.
    Naheshimu mchango wa timu hizi, ambao zinatoa wachezaji wengi timu ya taifa na hata kikosi cha sasa ukikitazama, wachezaji wote wametoka timu hizo, kasoro wawili tu, waliotoka Mtibwa Sugar.
    Sasa kama tunazitegemea timu hizi kutuzalishia wachezaji bora na zenyewe zinatuhumiana kwa michezo michafu, je soka yetu inaelekea wapi?  Kama timu yetu ya taifa, inaundwa na wachezaji ambao hawaziwezeshi timu zao kushinda kwa uwezo bali kwa kuachiwa na wapinzani, je soka yetu inaelekea wapi?
    Nadhani, umefika wakati sasa chombo chenye mamlaka ya juu katika soka ya Tanzania kikachukua hatua. Chombo hicho si kingine, bali Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Muda mrefu wadau wanapiga kelele, juu ya rushwa katika soka ya Tanzania na mara ya mwisho rais wa TFF, Leodegar Tenga akasema ni vigumu wao kupambana na rushwa bila ushirikiano na idara husika kwa maana ya jeshi la Polisi.
    Lakini kama Azam, Simba na Yanga zote zinachukua hatua dhidi ya wachezaji wao kwa madai ya kununuliwa, TFF inaona ugumu gani kulifanyia kazi suala hilo?
    Kama viongozi wa klabu wanawahukumu wachezaji bila ushahidi, TFF iwaite wote na kuwahoji kwa umakini, kuomba vielelezo na ushahidi walioutumia kuwachukulia hatua wachezaji hao.
    Kama ni ushahidi wa mazingira tu, au hisia basi viongozi watahitaji kuelimishwa. Nimependezewa kidogo na hatua ya Yanga, hawajawasimamisha wala kuwafukuza Berko na Mwasyika, bali wamewahamishia benchi na ikitokea wakapata nafasi tena wanaweza kujiuliza.
    Lakini Azam na Simba wamekwenda mbali zaidi- ila kitu rahisi kwangu kuamini hapa ni kwamba, inawezekana timu zote hizi zinafanyiana mchezo mchafu na mtu anapozidiwa kete, anachukua hatua ili kutengeneza kinga ya kesho.
    Wanaweza kuchukua hatua hata bila ushahidi wa kutosha, lengo tu ni kutengeneza mazingira ya wachezaji wengine kuogopa kesho kutumiwa. Ila sasa kwa staili hii soka yetu inaelekea wapi? Tutafakari na tuchukue hatua.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SOKA YETU INAELEKEA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top