Chuji kulia akimburuza kiungo wa JKT Mgambo juzi |
Na Mahmoud Zubeiry
KIUNGO wa Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’, amesema kwamba mechi
yao ya Jumapili dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itakuwa ngumu,
lakini watapigana kwa nguvu zao zote washinde ili kujiweka katika nafasi nzuri
kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana kutoka kambini
kwao, Bagamoyo mkoani Pwani, Chuji alisema kwamba Azam ni timu nzuri na ina
wachezaji wazuri, hususan katika nafasi ya kiungo, hivyo wanatarajia upinzani
mkali siku hiyo.
“Azam wazuri, wana viungo vizuri na mbaya zaidi wanapokuwa
wanacheza na sisi wanakomaa zaidi, wazi mchezo utakuwa mgumu,”alisema mtoto huyo
wa winga wa zamani wa CDA ya Dodoma, Iddi Athumani na kaka wa mshambuliaji wa
Coastal, Pius Kisambale.
Amesema anatarajia upinzani mkali kutoka viungo wa Azam kama
Salum Abubakar ‘Sure Boy’, lakini watakabiliana nao na watawaonyesha kwamba
Yanga ni zaidi.
“Tumepigana sana hadi kufika hapa, tulianza ligi vibaya, sasa
hivi tunataka kuiacha mbali kabisa Simba, kwa hivyo tumedhamiria sana kuwafunga
Azam Jumapili,”alisema Chuji.
Akiizungumzia Ligi Kuu kwa ujumla, Chuji alisema ni ngumu na
wanashukuru wao walianzia mechi ngumu zaidi za mikoani ambako walipokuwa wanapata
matokeo mabaya wengi waliwadharau na kuwakebehi.
“Sisi tumetoa droo na Prisons, tumefungwa na Mtibwa na Kagera
tukachekwa sana, sasa na wenzetu (Simba) wameenda mikoa miwili tu, lakini sasa
tunalingana pointi, kiko wapi sasa walichokuwa wanatucheka, hao hawajaenda
Kanda ya Ziwa, hawajaenda Arusha, hawajaenda Mbeya, unategemea nini?”alisema
Chuji.
Pamoja na hayo, Chuji amesema wanaamini mechi zote za Ligi
Kuu ni ngumu na wamejipanga kucheza kwa nguvu ile ile kila mechi, ili kuhakikisha
wanashinda zote zilizobaki.
Yanga itamenyana na Azam Jumapili Uwanja wa Taifa, mechi
ambayo inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua, kutokana na upinzani wa karibuni
baina ya timu hizo.