![]() |
| Na Mahmoud Zubeiry |
YOUTH ni wimbo mzuri
sana ambao wapenzi wa soka nchini sasa wamezoea kuusikia ukiimbwa na wadau
wengi wa soka nchini.
Kila tunapoanguka,
hata bila kutazama tulijikwaa wapi, wengi hushutumu tu kwamba tunakosa misingi-
na msingi mkubwa unaotajwa ni Youth, yaani vijana.
Wimbo huo kwa sasa
utashika tena chati, kufuatia, Simba SC, ikitumia kikosi chake cha vijana, kutwaa
ubingwa wa michuano mipya, BankABC Sup8R jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
baada ya kuifunga Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 4-3, katika mchezo uliodumu
kwa dakika 120.
Shujaa wa Simba jana
alikuwa ni Christopher Edward ambaye alifunga mabao matatu peke yake na
kufikisha jumla ya mabao tisa, hivyo kujinyakulia tuzo ya ufungaji bora wa
michuano hiyo na kuzawadiwa Sh. Milioni 2.
Hadi mapumziko, timu
hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba iliyotumia kikosi chake cha pili
kwenye michuano hiyo, Simba B ikitangulia kupata bao dakika ya 13, mfungaji
Christopher Edward aliyepokea pasi safi ya Ramadhan Singano ‘Messi’.
Mtibwa walisawazisha
bao hilo kwa penalti dakika ya 32, mfungaji Shaaban Kisiga ‘Malone’, baada ya
Jamal Mnyate kuangushwa kwenye eneo la hatari na Hassan Hatibu.
Mnyate hakuweza
kuendelea na mchezo baada ya pigo hilo na nafasi yake ikachukuliwa na Hassan
Seif.
Kipindi cha pili,
Simba inayofundishwa na Suleiman Matola, ilirudi kwa kasi tena na kufanikiwa
kupata bao la pili dakika ya 54, Edward akiunganisha krosi maridhawa ya Rashid
Ismail.
Dakika ya 57 Mtibwa
Sugar walisawazisha bao hilo kwa mpira wa adhabu nje kidogo ya eneo la penalti,
ambao ulipigwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’ na kumpita kipa Abuu Hashim,
aliyepewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano (MVP) na kuzawadiwa Sh. Milioni
2.5.
Simba ilipata bao la
tatu dakika ya 66, safari hii akifunga Haroun Athumani, kabla ya Hassan Seif
kuisawazishia Mtibwa dakika ya 79 kwa mpira wa adhabu tena, uliompita kirahisi
kipa mfupi Abuu.
Hadi dakika 90 za
mchezo huo zinamalizika, timu zote zilikuwa zimefungana mabao 3-3 na katika
dakika 30 za nyongeza, Edward aliihakikishia Simba B Sh. Milioni 40 na Kombe la
michuano hiyo mipya kwa bao lake safi dakika ya 112, akiunganisha pasi ya
Haroun.
Safari hii, Watoto wa
Matola hawakurudia kosa la kucheza rafu karibu na lango lao, walitulia na
kucheza soka ya kuonana kwa pasi nzuri za uhakika na kwenye shambulizi
wanabutua mpira, Mtibwa warushe na hadi kipyenga cha mwisho, Simba B waliibuka
vinara.
Mgeni rasmi, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara alikabidhi Kombe na
mfano wa Hundi, yenye thamani ya Sh. Milioni 40 kwa Nahodha wa Simba B, Hassan
Hatibu, wakati wachezaji wa timu hiyo, kila mmoja walipewa mfano wa Medali za
Dhahabu.
Mtibwa Sugar walipewa
Hundi ya Sh. Milioni 20 na mfano wa Medali za Fedha kila mmoja.
Katika mchezo huo,
kikosi cha Simba kilikuwa; Abuu Hashimu, William Lucian ‘Gallas, Omary Salum/ Jesse
Nyambo, Hassan Isihaka, Hassan Hatibu, Said Ndemla, Haroun Athumani, Abdallah
Seseme, Rashid Ismail, Edward Christopher na Ramadhan Singano ‘Messi’/Frank
Sekule.
Kwa ujumla, mwanzo hadi mwisho Simba haikufungwa hata mechi
moja, ikianza kutoa kwa sare ya 1-1 na Jamhuri ya Pemba katika mchezo wa kwanza
wa kundi lake, A, kabla ya kuzifunga Mtende FC na Zimamoto, zote za Zanzibar mabao
2-0 kila mechi, yote yakitiwa kimiani na Edward.
Simba B ilionyesha mchezo mzuri tangu mwanzo, vijana wake
wakicheza kwa kujiamini, wakicheza kama timu ambayo ipo na mwalimu na inafuata
maelekezo. Walicheza kama vijana waliotayarishwa, walioandaliwa na haya ni
matunda ya timu hiyo kukaa pamoja kwa muda mrefu, miaka isiyopungua miwili.
Simba B imewavutia wengi, baada ya kuvifunga vikosi vya
kwanza vya timu ngumu za Bara, Azam FC katika Nusu Fainali 2-0 na baadaye
Mtibwa katika fainali. Ile Simba A ya akina Sunzu, kama ingekutana na Mtibwa au
Azam zilizofungwa na Simba B, dhahiri mechi zingekuwa ngumu.
Wakati fulani niliwahi kuandika, kwamba kusajili wachezaji
wazuri ni jambo moja, na kuwa na timu nzuri ni jambo lingine. Ili uwe na timu
nzuri, lazima uiandae, timu lazima ikae pamoja kwa muda mrefu, wachezaji
wazoeane na wauzoee mfumo na hii ndiyo siri ya mafanikio ya timu ya vijana ya
Simba.
Mwaka juzi Simba B haikufanya vizuri sana kwenye Kombe la
Uhai, michuano inayoshirikisha timu za vijana za klabu za Ligi Kuu, lakini
mwaka jana ilibeba Kombe hilo.
Ukitazama wachezaji wa Simba waliobeba Kombe la BankABC,
wengi wao ni wale wale ambao wamekuwa wakiichezea timu hiyo katika Kombe la
Uhai kwa miaka mitatu sasa- kwa hiyo unaweza kuona safari ya timu hiyo inaanzia
mbali.
Tangu msimu uliopita, kocha wa Simba A, Mserbia Milovan
Cirkovick alianza kuwakomaza baadhi ya wachezaji wa Simba kwa kuwatumbukiza
kwenye kikosi chake cha kwanza, miongoni mwao ni Edward, Messi na Jonas Mkude,
ambaye inasikitisha kutokana na kuwa majeruhi, hajacheza mashindano haya.
Lakini kama nilivyosema, Watanzania wengi, wakiwemo viongozi
na baadhi ya wachambuzi uchwara wa nchi hii, hukumbuka kuimba Youth pale tu
tunapoanguka na wengi, hasa hao wachambuzi magirini wanapotosha kabisa maana ya
hiyo youth yenyewe.
Kuwa na akademi baab kubwa au programu nzuri ya vijana,
haimaanishi klabu itaacha kusajili- hapana. Inaaminika akademi bora zaidi
duniani wanayo Barcelona, ambayo hivi sasa wanahaha kusaka saini ya kiungo
Mcameroon, Alex Song kutoka Cameroon. Wa nini na wao wana akademi?
TP Mazembe ya DRC, wana akademi na wachezaji wake wa timu za
vijana wamekuwa wakienda hadi Ulaya kwa ziara za mafunzo, lakini na msimu
uliopita tu walisajili wachezaji wawili kutoka Tanzania, Mbwana Samatta na
Thomas Ulimwengu.
Sasa utamsikia mchambuzi uchwara analaani Simba au Yanga
kusajili, akitaka ziwe na akademi, eti ziepuke kusajili. Jamani, nani kasema
hili? Arsenal wana akademi nab ado wanasajili. Klabu ipi kubwa Ulaya haina
akademi? Na mbona zinasajili tena wachezaji wa gharama.
Kwa hivyo, hata Simba itaendelea kusajili tu pamoja na
programu yao ya vijana kuonekana inaendelea vizuri. Nini nataka kusema hapa,
tuache kuwa watu wa kukurupuka, lazima tuwe na hoja endelevu, mipango endelevu na
thabiti katika kutafuta suluhisho la matatizo ya soka yetu.
Leo wengi wanaoipongeza Simba SC kwa kuingiza timu B kwenye
michuano ya BankABC na kutwaa Kombe, ni wale ambao waliiponda Yanga ilipoingiza
timu B kwenye Kombe la Urafiki, kiasi cha ZFA (Chama cha Soka Zanzibar) kuamua
kuwafukuza wale vijana, baada ya kucheza mechi moja tu.
Nilitamani kuandika kitu, kulaani kitendo cha ZFA, lakini
kwa kuwa nafahamu siasa za nchi hii, nikaamua kuacha lipite. Naamini kabisa,
Yanga wangeingiza pia timu yao B kwenye michuano ya BankABC, kama wasingekuwa
na kumbukumbu ya kufukuzwa Zanzibar.
Sasa leo watu wanaimba, klabu nyingine ziige Simba SC,
lakini kwa sasa nchini klabu nyingi zina timu imara za vijana, mfano timu za
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) zote, Azam FC na hata Coastal Union- lakini
wanasahau kuna baadhi ya mashindano sera zake hazitaki vijana. Tunasema nini
kuhusu hili?
Mtazamo mkubwa katika soka yetu ni fedha na hiyo ni kwa
sababu ni mtazamo unaoishia kwenye kivuli chetu- hatujui kwamba, tunaweza
kutengeneza fedha nyingi kupitia mradi madhubuti wa soka ya vijana, utakaokuwa
na sera nzuri ya kitaifa.
Leo TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) litakataa vijana
katika mashindano yake, kwa sababu wanahofia kukosa mashabiki uwanjani na
kukosa fedha, lakini hawajasoma hisia za mashabiki wan chi hii.
Tangu Nusu Fainali, mashabiki wa Simba wamekuwa wakimiminika
kwa wingi tu uwanjani kushuhudia soka safi ya timu yao ya vijana, kwa sababu
wamehamasika na sasa hakuna shaka Simba B inauza.
Lakini hata Yanga B inaweza kuuza pia, iwapo itapewa fursa
ya kujenga imani kwa mashabiki wake, na hasa ikizingatiwa historia nzuri ya
klabu hiyo na soka ya vijana kuanzia mradi wa Profesa Victor Sanslescu miaka ya
1970 na marehemu Tambwe Leya baadaye miaka ya 1990.
Niliwahi kushauri, TFF kulikoni kuchukua uenyeji wa Kombe la
Challenge, kwa nini wasipiganie uenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa vijana, iwe U-17 au 20?
Nikasema kabisa, kwa sasa tuna mpango mzuri wa kuibua
wachezaji kupitia mashindano mengi ya vijana, lakini tatizo letu lipo katika
kuwaendeleza hatua kwa hatua hadi kuwakomaza katika kiwango cha kimataifa.
Uhai Cup sijui ni wiki moja au mbili, kadhalika BankABC
vijana wa Simba wamepiga kazi wiki mbili tu, sehemu nyingine ya msimu,
tunawafikiriaje hawa vijana, ambao klabu zinashurtishwa na kanuni kuwalea? Hatuoni
tunahitaji mashindano zaidi ya vijana ili kuwakomaza?
Pata picha, mchezaji anapigiwa wimbo wa taifa katika Fainali
za Vijana Afrika, lazima huyo atatamani kupigiwa na wimbo huo kwenye Fainali za
wakubwa za Afrika pia na hapo tutakuwa tunatengeneza chimbuko zuri la timu bora
ya taifa ya ushindani baadaye.
Miaka michache tu iliyopita, soka ya Tanzania ilikuwa juu ya
soka ya Botswana, lakini leo tunajivunia kucheza na Botswana kwamba tukipata
matokeo mazuri tutapanda kwenye viwango vya FIFA.
Naamini kwa mara nyingine, tumejifunza au kujikumbusha jambo
kuhusu soka ya vijana na wakati huu tukiipongeza Simba SC kwa kuingiza timu B
katika michuano hii na kubeba Kombe, itakuwa vema pia tukilaani kitendo cha ZFA
kuifukuza Yanga B kwenye Kombe la Urafiki. Eid Mubarak.



.png)
0 comments:
Post a Comment