![]() |
| Twite kulia akikabidhiwa jezi na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Bin Kleb |
Na Mahmoud Zubeiry
BEKI wa kimataifa wa
Rwanda, Mbuyu Twite mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
hatacheza mechi ya leo ya kirafiki kati ya timu yake mpya, Yanga dhidi ya African
Lyon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa sababu ameshindwa kuwasili nchini.
Na sasa kama ambavyo
BIN
ZUBEIRY iliwahi kuandika awali, beki huyo atajiunga na Yanga ikiwa Kigali,
Rwanda kwenye kambi fupi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara.
Habari za ndani
kutoka Yanga, zimesema kwamba tayari Twite amekwishazungumza hadi na kocha Mkuu
wa klabu, Mbelgiji Tom Saintfiet kumjulisha juu ya hilo. Kwa sasa, Mbuyu yupo
nyumbani kwao kwa asili, DRC kwa mapumziko mafupi kabla ya kuja kuanza maisha
mapya Jangwani.
Katika mchezo wa
leo, Yanga pia itamkosa mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Said Bahanuzi ‘Spider Man’, ambaye anasumbuliwa na maumivu ya goti.
Meneja wa Yanga,
Hafidh Suleiman aliiambia BIN ZUBEIRY mapema leo kwamba,
Bahanuzi anasumbuliwa na maumivu ya goti na leo atamuona daktari wa klabu, Dk
Sufiani Juma kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Saa mbili zijazo, Yanga
SC itashuka dimbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na African Lyon katika
mechi ya kirafiki, huo ukiwa mchezo wa kwanza wa kirafiki kwa Yanga, tangu
itwae ubingwa wa Kombe la Kagame mwezi uliopita na kwa wakati huo imekuwa
ikijifua tu kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Pamoja na kukosekana
kwa Twite na Bahanuzi, lakini mashabiki wa Yanga leo watapata fursa ya
kumshuhudia kwa mara ya kwanza, mshambuliaji Didier Kavumbangu waliyemsajili
kutoka Atletico Olimpique ya Burundi akiichezea timu yao.
Kavumbangu ndiye
aliyewafunga Yanga mabao yote mawili, walipomenyana na timu hiyo ya Burundi na
kulala 2-0 na kwa kuwa mfungaji bora wa Kagame, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ ni
mgonjwa, Didier lazima ataanza.
Tayari Yanga
imewasilisha usajili wake Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivyo kocha Tom
Saintfiet raia wa Ubelgiji anaweza kumpanga yeyote atakaye.
Kikosi kamili cha
Yanga ni; Makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said
Mohamed.
Mabeki; Shadrack Nsajigwa (Nahodha), Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar
Joshua, David Luhende na Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin
Yondan, Mbuyu Twite, Ibrahim Job na Ladislaus Mbogo.
Viungo; Athuman Idd ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’ na Salum Telela, Nizar
Khalfan, Shamte Ally, Idrisa Rashid, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Rashid Gumbo
na Nurdin Bakari.
Washambuliaji; Said Bhanaunzi ‘Spider Man’, Hamisi Kiiza ‘Diego’, Didier
Kavambagu na Jerry Tegete.
Kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Simon Msuva, wanaendelea kukomazwa
katika kikosi cha kwanza, wakitokea kikosi cha pili. Awali Yanga ilikuwa icheze
na Coastal Union, lakini mechi hiyo imefutwa.



.png)
0 comments:
Post a Comment