• HABARI MPYA

    Monday, August 20, 2012

    BAHANUZI 'SPIDER MAN' KUWAKOSA AFRICAN LYON LEO

    JEMBE TUTALIKOSA LEO; Bahanuzi 'Spider Man' kushoto akiwatoka mabeki wawili wa APR, kulia ni Twite wakati bado yupo APR.

    Na Mahmoud Zubeiry
    MFUNGAJI bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ hatacheza leo mechi ya kirafiki dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na maumivu ya goti.
    Meneja wa Yanga, Hafidh Suleiman ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Bahanuzi anasumbuliwa na maumivu ya goti na leo atamuona daktari wa klabu, Dk Sufiani Juma kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
    Yanga SC leo wanatarajiwa kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na African Lyon katika mchezo wa kirafiki, ambao imeelezwa beki Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda atacheza.
    Lakini mbaya zaidi hadi asubuhi hii, beki huyo alikuwa hajawasili nchini, ingawa BIN ZUBEIRY ilipowasiliana na kiongozi mmoja wa klabu hiyo, alisema ‘Shaka ondoa, utamuona Twite uwanjani leo’.
    Huo utakuwa mchezo wa kwanza wa kirafiki kwa Yanga, tangu itwae ubingwa wa Kombe la Kagame mwezi uliopita na kwa wakati huo imekuwa ikijifua tu kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
    Mbali na Twite, mashabiki wa Yanga leo pia watapata fursa ya kumshuhudia kwa mara ya kwanza, mshambuliaji Didier Kavumbangu waliyemsajili kutoka Atletico Olimpique ya Burundi.
    Kavumbangu ndiye aliyewafunga Yanga mabao yote mawili, walipomenyana na timu hiyo ya Burundi na kulala 2-0 na kwa kuwa mfungaji bora wa Kagame, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ ni mgonjwa, Didier lazima ataanza.
    Tayari Yanga imewasilisha usajili wake Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivyo kocha Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji anaweza kumpanga yeyote atakaye.
    Kikosi kamili cha Yanga ni; Makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed.
    Mabeki; Shadrack Nsajigwa (Nahodha), Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, David Luhende na Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Ibrahim Job na Ladislaus Mbogo.
    Viungo; Athuman Idd ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’ na Salum Telela, Nizar Khalfan, Shamte Ally, Idrisa Rashid, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Rashid Gumbo na Nurdin Bakari.
    Washambuliaji; Said Bhanaunzi ‘Spider Man’, Hamisi Kiiza ‘Diego’, Didier Kavambagu na Jerry Tegete.
    Kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Simon Msuva, wanaendelea kukomazwa katika kikosi cha kwanza, wakitokea kikosi cha pili. Awali Yanga ilikuwa icheze na Coastal Union, lakini mechi hiyo imefutwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAHANUZI 'SPIDER MAN' KUWAKOSA AFRICAN LYON LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top