• HABARI MPYA

    Monday, June 06, 2016

    AZAM ACADEMY MABINGWA MICHUANO YA AFRIKA MASHARIKI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam FC Academy’, usiku wa leo imefanikiwa kuwa mabingwa wa michuano ya vijana ya Afrika Mashariki ‘Azam Youth Cup 2016’ baada ya kuichapa Ligi Ndogo Academy kutoka Kenya mabao 3-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.
    Azam Academy inatwaa ubingwa huo ikiwa imefikisha jumla ya pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu ilizocheza nyingine zikiwa dhidi ya Future Stars Academy kutoka Arusha (4-1) na Football for Good Academy ya Uganda (5-1).
    Kikosi kizima cha Azam Academy na viongozi wao wakiwa na Kombe lao
    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba (kulia) akimkabidhi tuzo mchezaji Shaaban Iddi baada ya kuibuka mfungaji bora
    Shujaa wa mabingwa hao kwenye mchezo wa leo alikuwa ni mshambuliaji wake hatari Shaaban Idd aliyepachika wavuni mabao mawili kwa ustadi mkubwa dakika ya 15 na jingine 90, alilolifunga kwa staili ya ‘tik-tak’ huku bao jingine likifungwa na mshambuliaji mwingine hodari wa timu hiyo Yahaya Zaidi, katika dakika ya 27.
    Shaaban kufunga mabao hayo kunamfanya awe amefikisha matano na kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo huku Yahaya aliyekuwa akimfukuzia kwa kasi akiwa nayo manne.
    Ligi Ndogo waliopoteza pambano hilo wenyewe wamefanikiwa kushika nafasi ya tatu nyuma ya Football for Good Academy waliokamata nafasi ya pili huku Future Stars ikishika nafasi ya nne, timu zote hizo zikiwa zimekisanyia jumla ya pointi tatu lakini zimetofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD).
    Wakati Azam Academy ikiibuka mabingwa, pia baadhi ya wachezaji waliofanya vizuri kwenye kila idara waliweza kupewa tuzo binafsi kufuatia mafanikio hayo.
    Mshambuliaji wa Azam Academy, Shaaban Idd aling’ara katika utoaji tuzo hizo baada ya kutwaa tuzo mbili, ile ya ufungaji bora na mshambuliaji bora wa michuano hiyo baada ya kuwa kinara wa mabao akipachika matano huku Tuzo ya Beki Bora ikienda kwa beki wa Azam Academy, Abbas Kapombe, ambaye ni mdogo wa staa wa Azam FC, Shomari Kapombe.
    Tuzo ya Mchezaji Bora wa michuano hiyo imeenda kwa Stephen Bongomin wa Football for Good Academy na staa mwingine wa timu hiyo Allan Ganukupa, alitwaa Tuzo ya Kiungo Bora wa michuano hiyo huku ile ya Kipa Bora ikibebwa na Rodgers Siteti.
    Michuano hiyo iliyoandaliwa na Azam FC ni ya kwanza kufanyika nchini, ambapo itakuwa endelevu na itafanyika tena mwakani ikihusisha academy za nchi za Afrika Mashariki lengo ni kukuza kiwango cha soka cha nchi hizo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM ACADEMY MABINGWA MICHUANO YA AFRIKA MASHARIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top