• HABARI MPYA

    Saturday, August 13, 2016

    FIFA YAIFUNGULIA YANGA TMS SAA 48 IFANYE USAJILI HADI KESHO USIKU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limefungua mtandao wa usajili, ujulikanao kama Transfer Matching System (TMS) wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ili kutoa fursa kwa klabu ya Yanga kuingiza usajili wake.
    Hatua hiyo inafuatia ombi la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa FIFA, baada ya Yanga SC kuchelewa kutuma usajili wake katika siku ya mwisho Agosti 6, mwaka huu.
    Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo mjini Dar es Salaam kwamba dirisha la usajili la Bara limefunguliwa kwa saa 48 kuanzia leo.
    “Hii ni kuwataarifu kuwa, dirisha la usajili limefunguliwa na FIFA TMS kwa saa 48, hivyo litakuwa wazi mpaka Jumapili saa 6 usiku. Kwa taarifa zaidi, klabu ziwasiliane na Meneja wa TMS Jonas Kiwia,”alisema Mwesigwa.

    Dirisha la usajili kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza la StarTimes na Ligi Daraja la Pili msimu wa 2016/2017 lilifungwa saa 6.00 usiku wa Jumamosi Agosti 6, 2016 huku Yanga ya Ligi Kuu na Coastal Union ya Daraja la Kwanza zikiwa hazijatuma majina TMS, ambayo chombo chake cha kutunza kumbukumbu (server) kipo Makao Makuu ya FIFA mjini Zurich, Uswisi.
    TFF ikazitaka Yanga na Coastal kutuma utetezi wake wa kushindwa kusajili na kuupeleka FIFA kuomba dirisha hilo lifunguliwe tena, jambo ambalo limekubaliwa.
    Kwa kawaida mfumo huu upo chini ya FIFA na TFF hutoa taarifa kwa FIFA tarehe ya kufungua dirisha la usajili na kufunga.
    Mfumo huu uhusisha pande tatu ambazo ni klabu, shirikisho (TFF) na FIFA. Kimsingi kazi ya usajili hufanywa na klabu ambako inajaza fomu kwa njia ya mtandao na hupakia viambatanisho kama vile mikataba ya wachezaji na picha za wachezaji.
    Zoezi hili hufanywa na Meneja Usajili wa klabu husika wakati shirikisho hufanya kazi ya kuhakiki na kuidhinisha tu na FIFA huratibu na kuusimamia mfumo mzima. 
    Kabla ya kutangaza kufunguliwa kwa dirisha la usajili hapo Juni 15, 2016 Shirikisho liliandaa kozi ya mafunzo ya usajili kwa klabu zote 64 zikiwa ni 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara; 24 zitakazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza la StarTimes na timu 24 zitakazoshiriki Ligi Daraja la Pili msimu wa 2016/2017.
    Baadhi ya timu hazikutuma wawakilishi, lakini ziko zilizofanya jitihada za kuomba usaidizi kwa kufika ofisini TFF kuomba usaidizi wa kufanya usajili na zilifanikiwa. Kwa Yanga, licha ya kuwa hapa Dar es Salaam, haikuomba usaidizi wowote na hata walipokumbushwa kuhusu suala la usajili, hawakujibu kitu.
    Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo msimu wa 2014/2015 na 2015/2016, ni moja ya vilabu ambavyo havikutuma mwakilishi kwenye kozi iliyofanyika Uwanja wa Taifa kwa siku tatu mfululizo ikigusa wawakilishi wa madaraja ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
    Meneja wa TMS wa Yanga ni Katibu Mkuu ni Baraka Deusdedit ambaye hakuwahi kupata mafunzo ya TMS – lakini bahati nzuri kwake, FIFA imewafungulia tena dirisha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FIFA YAIFUNGULIA YANGA TMS SAA 48 IFANYE USAJILI HADI KESHO USIKU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top