![]() |
| Simba SC na Kombe lao |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC imetwaa
ubingwa wa michuano mipya, BankABC Sup8R jioni ya leo, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, baada ya kuifunga Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 4-3, katika mchezo
uliodumu kwa dakika 120.
Shujaa wa Simba hivi
leo, alikuwa ni Christopher Edward ambaye alifunga mabao matatu peke yake na
kufikisha jumla ya mabao tisa, hivyo kujinyakulia tuzo ya ufungaji bora wa michuano
hiyo na kuzawadiwa Sh. Milioni 2.
Hadi mapumziko, timu
hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba iliyotumia kikosi chake cha pili
kwenye michuano hiyo, Simba B ikitangulia kupata bao dakika ya 13, mfungaji
Christopher Edward aliyepokea pasi safi ya Ramadhan Singano ‘Messi’.
Mtibwa walisawazisha
bao hilo kwa penalti dakika ya 32, mfungaji Shaaban Kisiga ‘Malone’, baada ya
Jamal Mnyate kuangushwa kwenye eneo la hatari na Hassan Hatibu.
Mnyate hakuweza
kuendelea na mchezo baada ya pigo hilo na nafasi yake ikachukuliwa na Hassan
Seif.
Kipindi cha pili,
Simba inayofundishwa na Suleiman Matola, ilirudi kwa kasi tena na kufanikiwa
kupata bao la pili dakika ya 54, Edward akiunganisha krosi maridhawa ya Rashid
Ismail.
Dakika ya 57 Mtibwa Sugar
walisawazisha bao hilo kwa mpira wa adhabu nje kidogo ya eneo la penalti, ambalo
lilipigwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’ na kumpita kipa Abuu Hashim, aliyepewa
tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano (MVP) na kuzawadiwa Sh. Milioni 2.5.
Simba ilipata bao la
tatu dakika ya 66, safari hii akifunga Haroun Athumani, kabla ya Hassan Seif
kuisawazishia Mtibwa dakika ya 79 kwa mpira wa adhabu tena, uliompita kirahisi
kipa mfupi Abuu.
Hadi dakika 90 za
mchezo huo zinamalizika, timu zote zilikuwa zimefungana mabao 3-3 na katika
dakika 30 za nyingeza, Edward aliihakikishia Simba B Sh. Milioni 40 na Kombe la
michuano hiyo mipya kwa bao lake safi dakika ya 112, akiunganisha pasi ya
Haroun.
Safari hii, Watoto wa
Matola hawakurudia kosa la kucheza rafu karibu na lango lao, walitulia na
kucheza soka ya kuonana kwa pasi nzuri za uhakika na kwenye shambulizi wanabutua
mpira, Mtibwa warushe na hadi kipyenga cha mwisho, Simba B waliibuka vinara.
Mgeni rasmi, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara alikabidhi Kombe na mfano
wa Hundi, yenye thamani ya Sh. Milioni 40 kwa Nahodha wa Simba B, Hassan Hatibu,
wakati wachezaji wa timu hiyo, kila mmoja walipewa mfano wa Medali za Dhahabu.
Mtibwa Sugar walipewa Hundi
ya Sh. Milioni 20 na mfano wa Medali za Fedha kila mmoja.
Katika mchezo huo,
kikosi cha Simba kilikuwa; Abuu Hashimu, William Lucian ‘Gallas, Omary Salum/ Jesse
Nyambo, Hassan Isihaka, Hassan Hatibu, Said Ndemla, Haroun Athumani, Abdallah
Seseme, Rashid Ismail, Edward Christopher na Ramadhan Singano ‘Messi’/Frank
Sekule.
Mtibwa Sugar; Shaaban
Hassan Kado, Malikqa Ndeule (16), Yussuf Nguya (5), Salum Swedy (2), Salvatory
Ntebe (20), Babu Ally Seif (17)/Juma Mpakala, Jamal Mnyate (26)/ Hassan Seif
(11)/Ally Mohamed ‘Gaucho’, Awadh Juma (27), Hussein Javu (21), Shaaban Kisiga
‘Malone’ (29) na Vincent Barnabas (13)/Said Mkopi.



.png)
0 comments:
Post a Comment