• HABARI MPYA

    Tuesday, June 07, 2016

    PROFESA MSOLLA ATEULIWA KAMATI YA LESENI ZA KLABU YA TFF

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Profesa Mshindo Msolla ameteuliwa katika Kamati ya Leseni (Club Licensing Committee) ambayo ndiyo yenye jukumu la kupitia maombi ya leseni kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza na kutoa uamuzi kwa kuzingatia Kanuni ya Leseni ya Klabu.
    Uteuzi huo umefanywa jana na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais wake, Jamal Malinzi na Kamati hiyo inayoundwa kwa mara ya kwanza itakuwa chini ya Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga na Makamu wake Wakili Emmanuel Matondo.
    Profesa Msolla (kushoto) akiwa na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete (kulia)

    Kocha  Profesa Msolla anakuwa sehemu ya Wajumbe watatu wa Kamati hiyo, wengine wakiwa ni David Kivembele na Hamisi Kissiwa.
    Taarifa ya TFF leo imesema kwamba klabu zinatakiwa kuchukua fomu za maombi TFF ambapo baada ya kuzirejesha zitafanyiwa kazi ambapo zile zitakazokuwa zimekidhi matakwa ya Kanuni husika zitapatiwa leseni husika ili zishiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kwa msimu wa 2016/2017.
    Kwa klabu ambazo zitashindwa kukidhi matakwa ya leseni yanayolenga kuhakikisha mpira wa miguu unaendeshwa kwa weledi na kupiga vita upangaji matokeo katika maeneo matano ya wachezaji (sporting), viwanja (infrastructure), utawala (administrative and personnel), umiliki wa klabu (ownership) na fedha (financial), hazitapa leseni hivyo kutokuwa na sifa ya kushiriki ligi.
    Klabu ambazo zitanyimwa leseni na kutoridhika na uamuzi huo, zitakuwa na fursa ya kukata rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF. Kwa mujibu wa Ibara ya 5(3) ya Kanuni ya Leseni ya Klabu ya TFF, Kamati hiyo ndiyo inayosikiliza rufani zinazopinga uamuzi wa Kamati ya Leseni ya TFF.
    Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ni Wakili Alloyce Komba (Mwenyekit), Wakili Abdallah Gonzi (Makamu Mwenyekiti), Dk Francis Michael, Abdallah Mkumbura na Wakili Twaha Mtengela. Klabu zote zinahimizwa kuchukua fomu za maombi mapema ili kutoa muda wa kutosha kwa TFF kupitia maombi yao na kufanya uamuzi kwa wakati muafaka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PROFESA MSOLLA ATEULIWA KAMATI YA LESENI ZA KLABU YA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top