• HABARI MPYA

    Monday, July 10, 2017

    MAYANGA AMTEMA KIPA WA YANGA, AMCHUKUA ‘DOGO’ WA SERENGETI MECHI NA RWANDA

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KOCHA Salum Mayanga amemuondoa kipa wa Yanga, Benno Kakolanya katika kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kumchukua chipukizi, Ramadhani Kabwili kwa ajili ya mchezo wa kwanza dhidi ya Rwanda Jumamosi.
    Taifa Stars wataanza kampeni za kuwania kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee kwa mara ya pili baada ya mwaka 2009 nchini Ivory Coast kwa kumenyana na Amavubi Jumamosi Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Na baada ya kurejea jana nchini na ushindi wa tatu kwenye michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini, kocha Mayanga anayesaidiwa na Fulgence Novatus amefanya mabadiliko madogo kikosini.
    Ramadhani Kabwili (katikati) amechukua nafasi ya Benno Kakolanya Taifa Stars

    Langoni amemuondoa Kakolanya na kumchukua kipa wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki Fainali za Afrika nchini Gabon Mei mwaka huu, Kabwili aliyeonyesha uwezo mkubwa kwenye michuano hiyo.
    Katika mkutano wake na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Mayanga amesema kikosi cha wacheaji 24 kitaondoka leo jioni kwenda Mwanza kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.
    “Leo jioni tunatarajia kuondoka kuelekea mjini Mwanza kwa ajili ya kuweka kambi kwa muda wa takribani siku nne kujiandaa na kufanya mazoezi ya kutosha ili tarehe 15 tufanye vizuri katika mechi dhidi ya Rwanda,”amesema kocha huyo na mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar ya Morogoro.
    Kikosi kinachotarajiwa kuondoka leo kinaundwa na makipa Aish Manula, Said Mohammed na Ramadhani Kabwili.
    Mabeki; Shomari Kapombe, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Hamimu Abdul, Boniface Maganga, Salim Mbonde, Abdi Banda na Nurdin Chona.
    Viungo; Muzamil Yassin, Himid Mao, Salmin Hoza, Raphael Daud, Erasto Nyoni, Said Ndemla, Simon Msuva, Shiza Kichuya na Joseph Mahundi.
    Washambuliaji ni Athanas Mdamu, John Bocco, Kelvin Sabato na Stahmil Mbonde.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAYANGA AMTEMA KIPA WA YANGA, AMCHUKUA ‘DOGO’ WA SERENGETI MECHI NA RWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top