• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 24, 2017

  WAKALI WA SIMBA TAIFA STARS KWENDA AFRIKA KUSINI KESHO

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI wa klabu ya Simba waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wanatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda mjini Johannesburg, Afrika Kusini kujiunga na kambi ya timu yao kwa maandalizi ya msimu mpya.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba wachezaji hao ni makipa Aishi Manula, Said Mohammed, mabeki Shomari Kapombe, Salim Mbonde, viungo Erasto Nyoni, Muzamil Yassin, Shiza Kichuya, Said Ndemla na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’.  
  Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Omog akiwa na wasaidizi wake katika kambi ya Afrika Kusini 
  Taifa Stars iliondolewa mapema kwenye michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayoshirikisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Rwanda Uwanja wa Kigali, uliopo Nyamirambo mjini Kigali Jumamosi.
  Matokeo hayo yanamaanisha Taifa Stars inaondolewa kwa bao la ugenini, kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumamosi ya wiki iliyotangulia.
  Na baada ya matokeo hayo, wachezaji wa kikosi cha kocha Salum Mayanga, ambacho wiki mbili zilizopita kilishinda Medali ya Shaba kwenye michuano ya COSAFA Castle mjini Rusternburg, Afrika Kusini wanarejea kwenye klabu zao kwa maandalizi msimu mpya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAKALI WA SIMBA TAIFA STARS KWENDA AFRIKA KUSINI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top