• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 30, 2017

  YALIYOPITA SI NDWELE, KILA LA HERI, MESSI, MSUVA... KAFANYENI KAZI MOROCCO WAWATAMBUE

  KLABU ya Difaa Hassani El-Jadida ya Ligi Kuu ya Morocco imenunua mawinga wawili wa kimataifa wa Tanzania, Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ na Simon Happygod Msuva.
  Messi, mchezaji wa zamani wa Simba alitangulia kwenda Morocco mwezi uliopita akitokea Azam FC na Msuva akafuatia juzi usiku akikamilisha uhamisho wake kutoka Yanga, zote za Dar es Salaam.
  Hata hivyo, si Difaa wala wachezaji wenyewe walioweka wazi ni mikataba ya miaka mingapi, wachezaji watakuwa wanalipwa kiasi gani na klabu zao zimepata kiasi gani.  
  Messi aliibukia kikosi cha vijana cha Simba mwaka 2011 kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza – mwaka juzi akaondoka kwenda Azam FC ambayo imekuwa daraja lake la kwenda nje. 
  Msuva alijiunga na Yanga SC mwaka 2012 akitokea Moro United iliyokuwa tayari imehamishia maskani yake Dar es Salaam kutoka Morogoro na awali ya hapo alipitia akademi ya Azam baada ya kuibuliwa na iliyokuwa taasisi ya Pangollin ya kocha Charles Boniface Mkwasa, ambaye sasa ni Katibu wa Yanga, klabu aliyoichezea na kuifundisha awali. 
  Baada ya kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mfungaji bora mara mbili – bila shaka sasa ni wakati mwafaka kwa Msuva kwenda kutafuta changamoto mpya nje ya nchi. 
  Na Messi baada ya kucheza klabu mbili kubwa Tanzania, Simba na Azam hapana shaka ni uamuzi sahihi kuvuka mpaka wa Tanzania kwenda kujaribu maisha mengine yaa kisoka.
  Timu hiyo yenye maskani yake mji wa El Jadida ikiwa inatumia Uwanja wa El Abdi inataka kuwatumia mawinga wa Tanzania kujaribu kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Morocco, inayojulikana kama Botola, moja ya Ligi bora kabisa barani Afrika.
  Na Habari za Msuva na Messi kununuliwa na Difaa, zinakuja siku chache baada ya beki mwingine Mtanzania, Abdi Hassan Banda kununuliwa na Baroka FC ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
  Watatu hawa wanafanya idadi ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka ya ushindani nje ya nchi kufika saba, baada ya washambuliaji Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu wa AFC Eskilstuna ya Sweden, Elias Maguri wa Dhofar na Danny Lyanga wa Fanja, zote za Oman.
  Hizi ndizo habari ambazo mashabiki wa soka ya Tanzania wanapenda kusikia, wachezaji wa nchi yao wanacheza nje.
  Na wanapenda idadi iongezeke maradufu na hata ifike wakati, timu ya taifa ikiitwa wanasheheni wachezaji wanaocheza nje ili ifike wakati na sisi tuwe kama baadhi ya nchi nyingine za Afrika.
  Ifike wakati kikiitwa kikosi kwa ajili ya mechi za CHAN basi iwe rahisi kujua hiki ni cha wachezaji wa Ligi ya nyumbani tu, na kikiitwa cha AFCON basi kiwe na sura nyingi za vijana wanaocheza nje.
  Sivyo kama ilivyo sasa, ni Mbwana Samatta tu ndiye anatengeneza tofauti ya kikosi cha Taifa Stars cha CHAN na AFCON – tunahitaji namba kubwa ya wachezaji wanaocheza nje ili kukuza kiwango cha timu yetu ya taifa.
  Zipo hadithi za kusikitisha za kihistoria katika soka ya nchi hii, miaka ya 1970 hadi 1990 wachezaji wengi walizuiwa kwenda kucheza nje na matokeo yake tukashindwa kujenga misingi ya Watanzania kucheza nje kwa wingi.
  Wenzetu wa Afrika Magharibi waliochangamkia fursa hizo wakati huo sasa hivi wanajivunia mno biashara hiyo. Kama Iddi Paz ‘Father’ asingezuiwa kwenda Ligue 1 ya Ufaransa mwaka 1986, leo kungekuwa na Watanzania wangapi nchini humo?
  Iliwezekana vipi Nonda Shabani kucheza Ulaya na kufikia mafanikio makubwa na ikashindikana kwa aliyekuwa mshambuliaji wake namba moja Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’?
  Unaambiwa Edibily Lunyamila aliondoka Ujerumani katika umri usiozidi miaka 23 akiwa katika nafasi ya kusajiliwa na kurudi Tanzania kucheza Yanga.
  Athumani China aliondoka Uingereza naye arudi Yanga – kama ilivyokuwa kwa Haruna Moshi ‘Boban’ aliondoka Sweden akarudi Tanzania kucheza Simba. Victor Costa naye aliondoka Afrika Kusini akarudi Tanzania kucheza Simba.
  Ni hadithi za kusikitisha ambazo zinaumiza tu roho, kwani ndizo zimechangia kuzorota kwa soka yetu, kutoka kuwa nchi tishio kwa ukanda wetu enzi za Gossage Cup hadi kuwa vibonde zama hizi.
  Leo Tanzania inaondolewa na Rwanda kwenye mashindano ya mpira. Leo wachezaji wa Rwanda wanakuja kucheza mpira wa kutustaajabisha sisi Watanzania.
  Namna hii lazima watu waendelee kuwakumbuka akina Sunday Manara ‘Kompyuta’, Mtanzania wa kwanza kucheza Ulaya na mafundi mengine kama akina Abdallah Kibadeni na hao akina Lunyamila, Nteze John na wengine wengi tu.
  Wahenga walisema; “Yaliyopita si ndwele”, basi kwa sasa tusahau yaliyopita na tufurahie habari za Messi na Msuva kununuliwa Morocco wakijiwekea rekodi ya kuwa Watanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya nchi za Kaskazini mwa Afrika. Kila la heri vijana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YALIYOPITA SI NDWELE, KILA LA HERI, MESSI, MSUVA... KAFANYENI KAZI MOROCCO WAWATAMBUE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top