• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 25, 2017

  YANGA YAMPA MIAKA MIWILI KIPA WA SERENGETI BOYS, KESHO YAENDA KAMBINI MOROGORO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imemsajili kwa mkataba wa miaka miwili aliyekuwa kipa wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Ramadhani Awam Kabwili wenye kipengele cha kuongezewa miaka mitatu atakapofikisha umri wa miaka 18.
  Mlinda mlango huyo atakayetimiza umri wa miaka 17 Desemba 11, mwaka huu alidaka mechi zote za Serengeti Boys kwenye Fainali za Vijana Afrika chini ya umri wa miaka 17 nchini Gabon na kusifiwa mno kwa kiwango kizuri alichoonyesha.
  Kocha wa Yanga, Mzambia George Lwandamina ameridhika na uwezo wa kipa huyo na kuamua kumpa mkataba mrefu, aliosainiwa na walezi wake kwa sababu bado hajatimiza umri wa miaka 18.

  Ramadhani Kabwili amesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano Yanga

  Na Kabwili anaungana na kipa mwingine mpya, Mcameroon Youthe Rostand aliyesajiliwa kutoka African Lyon na Benno Kakolanya ambaye anakwenda kwenye msimu wa pili tangu asajiliwe kutoka Prisons ya Mbeya msimu uliopita.
  Kabwili na Rostand wote wanasajiliwa kuchukua nafasi za makipa wa muda mrefu wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’ waliomaliza mikataba yao na kuruhusiwa kuondoka.
  Yanga SC, mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wanaendelea na mazoezi kwa siku ya tatu leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kujiandaa na msimu mpya.  
  Wakati huo huo: Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga wanatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kesho kwenda mkoani Morogoro kuweka kambi ya siku saba kujiandaa na michezo miwili ya kirafiki itakayopigwa Agosti 6 na 12, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA YAMPA MIAKA MIWILI KIPA WA SERENGETI BOYS, KESHO YAENDA KAMBINI MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top