• HABARI MPYA

  Monday, July 31, 2017

  TFF YASHUSHA ADA ZA WACHEZAJI WA KIGENI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  ADA ya wachezaji wa kigeni kucheza Tanzania imepunguzwa kutoka Sh. Milioni 4.5 hadi Sh. Milioni 2 kwa kila mchezaji kuanzia msimu ujao unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi ujao, imeelezwa.
  Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyokutana Jumapili (Julai 30, 2017) katika Ukumbi wa Hosteli za shirikisho hilo Uwanja wa Karume, Ilala Jijini Dar es Salaam.
  Taarifa ya TFF kwa vyombo vya Habari leo imesema kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya 57 (5); Mchezaji yeyote wa kigeni anayesajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara atalipiwa ada maalumu ya Sh Milioni 2 kwa msimu kwa kila mchezaji ili usajili wake uthibitishwe na kuruhusiwa kucheza.

  Mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma anaingia katika msimu wake wa tatu Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 

  Gharama hizo ni punguzo la nusu ya gharama za awali, ambazo zilikuwa ni dola za Kimarekani 2,000, zaidi ya Sh. 4.5 kwa mchezaji mmoja. 
  Kikao hicho kimeagiza kuanzia msimu wa 2017/18 mchezaji atayesajiliwa hatapewa leseni ya kumruhusu kucheza mashindano husika kama vile Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL), Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kama hatakamilisha masharti makuu matatu kwa mujibu wa kanuni.
  Masharti hayo ni kukatiwa Bima ya Matibabu, Kuidhinishwa afya yake ambayo mara baada ya fomu yake kupitishwa na Kamati ya Tiba ya TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 18 (1) ya Ligi Kuu na Mkataba wake wa maandishi ‘hardcopy’ kuwasilisha TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 69 (8) ya Ligi Kuu.
  Kama kuna timu haitakidhi japo sharti moja kati ya hayo, basi mchezaji wake hatapewa leseni ya kucheza kwa msimu husika. 
  Hayo yamekuja baada ya klabu kutakiwa kuwawekea Bima ya Matibabu kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) inayosema: “Kila Klabu ina wajibu wa kuwawekea wachezaji wake bima ya matibabu na fidia kutokana na ajali michezoni. Klabu itakayokiuka kanuni hii itakuwa imepoteza sifa ya kuwa klabu ya Ligi Kuu, na usajili wa wachezaji wa timu yake hautathibitishwa na haitashirikishwa katika Ligi Kuu.
  Kuhusu Mikataba kwa mujibu wa Kanuni ya 69 (8), Kamati ya Utendaji imekubaliana kwamba: “Mikataba yote ya wachezaji ambao haujasajiliwa na kuthibitishwa na TFF, hautatambuliwa.”
  Kadhalika, sasa kwa mujibu wa kanuni ya 13 (6) Klabu Mwenyeji itakuwa na nafasi ya kuweka mpaka mabango 10 ya Mdhamini/Wadhamini wake. Ukubwa wa bango moja lile lenye vipimo vya 6m x 1m. 
  Kama timu ni mgeni katika mchezo husika, ana uwezo kufanya makubaliano na mwenyeji wake akampa nafasi katika hayo 10 ambayo yameruhusiwa kikanuni.
  Aidha, Kanuni ya 14 imeongezwa kipengele kimoja. Kanuni ya 14 (48) Klabu ina wajibu wa kushirikiana na mdhamini wa matangazo ya televisheni ikiwemo kupata picha za wachezaji na benchi la ufundi kwa ajili ya maandalizi ya mechi zao.
  Na Kanuni 14 (49), inasema: TFF/TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wo wote wa taratibu za mchezo kama zilivyoanishwa kwenye Kanuni ya 14 kwa kutoa onyo kali au karipio au kutoza faini kuanzia Sh. 200,000 (lakini mbili) mpaka Sh. 300,000 (laki tatu), na/au kufungia mchezo isiyozidi mitatu (3) au kipindi kisichozidi miezi mitatu (3) kwa mchezaji, kiongozi au timu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YASHUSHA ADA ZA WACHEZAJI WA KIGENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top