• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 28, 2017

  BANDA AWATEMBELEA SIMBA KAMBINI AFRIKA KUSINI...ILIKUWA RAHA SANA

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  ALIYEKUWA beki wa Simba, Abdi Hassan Banda leo ametembelea kambi ya timu hiyo mjini Johannesburg nchini ya Afrika Kusini na kusalimiana na wachezaji wenzake wa zamani. 
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Afrika Kusini, Banda amesema kwamba ataendelea kuithamini na kuiheshimu Simba SC kwa sababu ndiyo timu yake nyumbani iliyompa mafanikio hadi kuonekana nchini humo.
  “Ni timu ambayo imenipa mimi njia ya mafanikio, halafu wapo mji ambao mimi nipo (Johannesburg), hivyo nikaona ni vizuri niende kuwaona japo kuwasalimu wachezaji wenzangu, walimu na viongozi waliokuja na timu, hiyo ndiyo furaha yangu,”alisema Banda.
  Abdi Banda (kulia) akiwa na mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo katika kambi ya Simba Afrika Kusini
  Banda amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Baroka ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini mapema mwezi huu baada ya kung’ara katika michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini akiiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu.
  Banda alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza michuano ya COSAFA Castle na kutwaa Medali ya Shaba baada ya ushindi wa penalti 4-2 Julai 7, mwaka huu dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, tena akipiga moja ya matuta hayo manne.
  Simba imeweka kambi nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya na inatarajiwa kurejea nchini siku chache kabla ya tamasha lake maalum la kila mwaka, Simba Day, ambalo litafanyika Agosti 8, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Siku hiyo Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajiwa kutambulisha kikosi chao kipya cha msimu mpya pamoja na kuuza za wachezaji wake mbalimbali nyota.
  Abdi Banda akiwa na mshambuliaji Juma Luizio
  Shauku ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo ni kumuona aliyekuwa kiungo wa Yanga kwa miaka minne iliyopita, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima raia wa Rwanda ameondoka mwezi huu na anatarajiwa kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi.
  Pamoja na Haruna, wana Simba wana hamu ya kumuona tena mshambuliaji Emmanuel Okwi aliyetarajiwa kuingia kambini leo akiwa katika jezi ya Simba, baada ya kurejeshwa msimu huu kwa mara ya tatu.
  Nyota wengine wapya waliosajiliwa ni makipa Said Mohammed kutoka Mtibwa Sugar, Emanuel Mseja kutoka Mbao FC, Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni kutoka Azam FC, Jamal Mwambeleko kutoka Mbao, Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans, Ally Shomary kutoka Mtibwa Sugar na mshambuliaji John Bocco kutoka Azam FC 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BANDA AWATEMBELEA SIMBA KAMBINI AFRIKA KUSINI...ILIKUWA RAHA SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top