• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 24, 2017

  MSUVA KWENDA MOROCCO JUMATANO KUKAMILISHA UHAMISHO WAKE DIFAA EL-JADIDA

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM 
  WINGA wa Yanga SC, Simon Msuva anatarajiwa kuondoka nchini Jumatano kwenda Morocco kwa ajiloi ya kukamilisha uhamisho wake kujiunga na Difaa Hassani El-Jadida ya Ligi Kuu ya nchini humo.
  Difaa ambayo tayari imekwishamchukua Mtanzania mwingine, winga pia Ramadhani Singano ‘Messi’ kutoka Azam FC iko tayari kutoa dola 150,000 kumnunua Msuva ambaye amebakiza miezi tisa katika mkataba wake Yanga.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Msuva amesema kwamba akifuzu vipimo vya afya atasaini moja kwa moja mkataba wa kujiunga na timu hiyo ya Ligi Kuu ya Morroco.
  Simon Msuva anatarajiwa kwenda Morocco Jumatano kukamilisha uhamisho wake Difaa El-Jadida 

  Msuva amerejea Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo kutoka mjini Kigali alipokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo na wenyeji, Rwanda kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN.
  Taifa Stars imeondolewa mapema kwenye michuano ya CHAN, inayoshirikisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 juzi na wenyeji Rwanda Uwanja wa Kigali, uliopo Nyamirambo mjini Kigali, hivyo kuondolewa kwa bao la ugenini, kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumamosi iliyopita.
  “Ninamshukuru Mungu nimerudi salama kutoka Rwanda na Jumatano ninaanza safari ya kuelekea nchini Morocco kumalizia taratibu zilizobakia,”alisema Msuva aliyejiunga na Yanga mwaka 2012 akitokea Moro United.
  Timu hiyo yenye maskani yake mji wa El Jadida ikiwa inatumia Uwanja wa El Abdi inataka kuwatumia mawinga wa Tanzania kujaribu kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Morocco, inayojulikana kama Botola, moja ya Ligi bora kabisa barani Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MSUVA KWENDA MOROCCO JUMATANO KUKAMILISHA UHAMISHO WAKE DIFAA EL-JADIDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top