• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 30, 2017

  RASMI, RAPHAEL DAUDI LOTH NI MCHEZAJI MPYA WA YANGA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imefanikiwa kukamilisha uhamisho wa kiungo chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Raphael Daudi Loth kutoka Mbeya City.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika amesema kwamba kiungo huyo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesaini mkataba wa miaka miwili kuhamia timu ya Dar es Salaam.
  “Tunafurahi kuwatangazia wana Yanga kwamba tumefanikiwa kukamilisha usajili wa kiungo wa Raphael Daudi kutoka Mbeya City ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili,”amesema.
  Raphael Daudi Loth akisaini mkataba wa miaka miwili Yanga SC kutoka Mbeya City

  Na Daudi anakuwa mchezaji wa nane mpya kusajiliwa Yanga SC katika dirisha hili hadi sasa, baada ya makipa Mcameroon Youth RostandE kutoka African Lyon iliyoshuka Daraja, Ramadhan Kabwili aliyepandishwa kutoka timu B, beki Abdallah Hajji kutoka Taifa Jang’ombe, viungo Pius Buswita kutoka Mbao FC, Papy Kabamba Tshishimbi, Mkongo kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland, Hussein Akilimali huru na mshambuliaji Ibraahim Hajib kutoka Simba.
  Loth alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza michuano ya COSAFA Castle na kutwaa Medali ya Shaba baada ya ushindi wa penalti 4-2 Julai 7, mwaka huu dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg.
  Baada ya kusaini mkataba huo, Loth anakwenda moja kwa moja kambini Morogoro kujiunga na wenzake kwa maandalizi ya msimu mpya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RASMI, RAPHAEL DAUDI LOTH NI MCHEZAJI MPYA WA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top