• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 24, 2017

  HIMID MAO AAMUA KUSHUGHULIKIA MIPANGO YA KUTOKA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BAADA ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kutolewa kwenye mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), Nahodha Himid Mao Mkami amesema sasa anaelekeza nguvu zake katika kushughulikia uhamisho wake nje ya nchi.
  Taifa Stars imeondolewa mapema kwenye michuano ya CHAN, inayoshirikisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 juzi na wenyeji Rwanda Uwanja wa Kigali, uliopo Nyamirambo mjini Kigali, hivyo kuondolewa kwa bao la ugenini, kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumamosi iliyopita.
  Himid Mao sasa anaelekeza nguvu zake katika kushughulikia uhamisho wake nje ya nchi

  Na katika mahojiano na Bin Zubeiry Sports – Online, Mao amesema kwamba ameumiza na matokeo hayo, lakini ndiyo soka hivyo wanasahau yaliyopita na wanaelekeza nguvu katika changamoto zilizo mbele yao.
  “Katika soka likitokea la kuumiza leo, unasahau mara moja na kusonga mbele, kwa sababu siyo mwisho, Mpira unaendelea na mashindano yanaendelea, tutaajaribu bahati yetu wakati mwingine,”alisema.
  Pamoja na hayo, Himid akasema kwamba kwa sasa anawasiliana na wakala wake ili kujua mustakabali wake wa msimu ujao, kwa sababu kuna ofa nyingi wamepata.
  “Tangu wakati nipo Afrika Kusini kwenye COSAFA hizo ofa zilikuwepo, sasa wakala yeye alikuwa anazifanyia kazi, nataraji sasa atakuwa amekwishapata majibu, nitawasiliana naye ili kujua,”alisema mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Mtibwa Sugar ya Morogoro.   
  Himid amesema ana ofa kutoka Misri, Afrika Kusini na Denmark ambako alikwenda kufanya majaribio Aprili mwaka huu, hivyo anasubiri kusikia kutoka kwa wakala wake ili kujua mustakabali wake wa msimu ujao.
  Himid Mao anatarajiwa kumaliza mkataba wake Azam FC Novemba mwaka huu na mwenyewe ameonyesha dhamira ya kutotaka kubaki kabisa nchini, licha ya pia kuhusishwa na mpango wa kuhamia kwa wapinzani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HIMID MAO AAMUA KUSHUGHULIKIA MIPANGO YA KUTOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top