• HABARI MPYA

    Thursday, May 16, 2013

    YANGA NA JINAMIZI LA 5-0 MEI 6 MWAKA JANA TAIFA, MANJI…


    Na mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 15, 2013, SAA 12:00 ASUBUHI
    NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zinatarajiwa kuwaka moto keshokutwa, Jumamosi (Mei 18, 2013) kwa mpambano wa watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga. Huo utakuwa mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wakiwa tayari wamewavua ubingwa wapinzani wao wa jadi, Simba SC. BIN ZUBEIRY inaendelea kukuletea mfululizo wa makala za kuelekea pambano hilo linalobeba picha halisi ya soka ya Tanzania na leo tunahamia kwenye dhamira ya Yanga kutaka kulipa kipigo cha mabao 5-0 katika mechi ya kufunga msimu uliopita. Endelea.
    Manji kulia na Waziri Mkuchika

    MARA kadhaa, Mwenyekiti wa Yanga, Alhaj Yussuf Mehboob Manji amekaririwa akisema, anaumziwa kichwa na kisasi cha 5-0 na alikuwa katika wakati mgumu zaidi, kipindi ambacho timu ilikuwa ikipata ushindi mwembamba katika mechi zake za Ligi Kuu msimu huu.
    Manji alisema wachezaji wa Yanga lazima waonyeshe tofauti na wachezaji wa timu nyingine, baada ya kupatiwa kila kitu kinachowafanya wawe bora zaidi, ikiwemo maslahi mazuri, kupelekwa ziara ya mafunzo Uturuki kwa wiki mbili na pia kuwa chini ya mwalimu bora, Mholanzi Ernie Brandts.
    Manji alisema wazi Machi mwaka huu kwamba ukame wa mabao katika klabu hiyo unamnyima usingizi haswa akilifikiria deni la kufungwa 5-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
    Alisema hayo makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam wakati wa kutambulisha Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo. Alisema kwamba amekwishazungumza na Benchi la Ufundi, chini ya kocha Mkuu, Brandts ambaye ni beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, ambalo lilimuahidi kulifanyia kazi tatizo hilo.
    “Benchi la ufundi linafanyia kazi tatizo hilo, lakini hatuwezi kuona matunda yake ndani ya siku mbili, itachukua muda, ila kwa kweli inanichanganya sana,”. “Sisi viongozi tumefanya juhudi zetu kusajili wachezaji wazuri na benchi zuri la Ufundi, tumeleta kocha bora, wachezaji wanaishi vizuri, wanapata maslahi mazuri. Sasa iliyobaki ni wao wafanye kazi,”.
    “Lakini tunakwenda mechi nne sasa, timu inashinda bao moja, moja, timu tumeipeleka Ulaya, Uturuki kufanya kambi, inarudi hapa, haionyeshi tofauti na timu nyingine,”. “Tunapata bao dakika ya sabini na…, tukipata dakika ya thelathini na…, inakuwa kucheza kwa wasiwasi hadi mpira uishe, sasa kwa nini. Inatakiwa tushinde goli tatu, ukishinda goli tatu au zaidi, mpinzani akikutana na wewe anafikiria kupunguza iwe mbili, sasa kwa kweli inachanganya,”alisema Manji.
    Kweli, kama alivyosema Manji, ikiwa una deni la Sh. 100,000 na wewe hauna hata Sh. 20,000, lazima kichwa kikuume na katika siku za karibuni, viongozi, benchi la ufundi na hata wachezaji wa Yanga wanaonekana kufuta ndoto za kulipa 5-0 na badala yake wanachotaka ni ushindi tu.
    “Mimi kama mchezaji, matokeo yoyote yanatokea, ila hatuwezi kukubali kufungwa tena na Simba, itaonekana wao wanatuweza sana, sizungumzii idadi ya mabao, cha muhimu ni pointi tatu, mabao matano ni vizuri tukirudisha,”hiyo ni kauli ya kiungo tegemeo wa klabu hiyo, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima hivi karibuni akizungumza na BIN ZUBEIRY.
    Kipigo cha 5-0 mwaka jana kwa kiasi kikubwa kilichangiwa na mgogoro uliokuwapo, baina ya Wazee wa klabu hiyo chini ya kinara wao, Ibrahim Akilimali dhidi ya uongozi uliokuwapo madarakani chini nya Mwenyekiti Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na kuna imani kwamba wachezaji walitumiwa kucheza chini ya kiwango ili kufanikisha mpango wa kuung’oa madarakani uongozi.
    Katikati Simba SC walikuwa wanakabiliwa na mgogoro wa uongzozi pia ambao umechangia timu kupoteza ubingwa na kukosa hata nafasi ya pili. Kulikuwa kuna dalili za Yanga kulipa 5-0 kama mgogoro huo usingeisha. Sasa mgogoro umeisha Simba SC na umoja umerudi, nao baada ya kukosa ubingwa na nafasi ya pili, wanataka wajenge heshima ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya watani wao, Yanga Jumamosi.
    Leo, uongozi na wadau kadhaa wa klabu hiyo, likiwemo kundi la Friends of Simba wanakwenda Zanzibar kufanya mazungumzo na wachezaji wa timu yao walioko kambini huko. Wazi, huko wachezaji pamoja na kupewa motisha ili kuwajenga kisaikolojia kuelekea mechi hiyo, pia watatangaziwa na ahadi nono iwapo watashinda Jumamosi.
    Wazi, kulipa 5-0 kwa Yanga sasa kama ambavyo wao wenyewe wameanza kukata tamaa, litakuwa jambo gumu, japo katika soka lolote huweza kutokea.

    Mambo yalivyokuwa Mei 6, Taifa hadi 5-0
    Nsajigwa akijaribu kumdhibiti Okwi
    ILIKUWA ni Mei 6, mwaka 2012 wakati Wekundu wa Msimbazi, Simba SC walipokabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa shangwe nzito, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuwabwaga wapinzani wao wa jadi, Yanga mabao 5-0.
    Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi mawili, Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mutesa Mafisango.
    Hicho kilikuwa kipigo cha pili kikali kihistoria Simba wanaifunga Yanga, baada ya zile 6-0 za mwaka 1977.
    Ilikuwa ni hoi hoi, nderemo na vifijo kuanzia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi kona mbalimbali za Jiji, rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimetawala na shangwe za Simba.
    Hadi mapumziko, Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya pili tu ya mchezo huo.
    Okwi alimtungua kipa Mghana, Yaw Berko baada ya kutumia mwanya wa kuzubaa kwa mabeki wa Yanga mwanzoni mwa mchezo huo.
    Katika kipindi hicho, Okwi alikuwa akimpita kwa urahisi beki mkongwe wa Yanga, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele ambaye aliishia kumkwatua mara kwa mara, jambo ambalo lilimponza kwenda chumba cha kupumzikia akiwa ana kadi moja ya njano aliyopewa dakika ya 39.
    Pamoja na kufungwa bao hilo, Yanga waliendelea kucheza kwa utulivu, wakigongeana pasi vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa, ingawa kikwazo kilikuwa Tanzania One, Juma kaseja.
    Nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho na ambayo Yanga wataijutia waliipata dakika ya 35, baada ya Mwanasoka Bora wa Uganda, Hamisi Kiiza kuwatoka vizuri mabeki wa Simba, lakini akiwa amebaki yeye na kipa, hesabu zake ziliendana na Kaseja.
    Kiiza aliupelekea mpira upande wa kushoto wa kipa huyo bora Tanzania, ambaye naye akachupa upande huo huo na kuokoa.
    Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko, wakimtoa kipa Yaw Berko na kumuingiza Said Mohamed Kasarama, wakati Simba walimpumzisha Mwinyi Kazimoto na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.
    Simba waliingia tena kwa kasi na kufanikiwa kupata mabao matatu ya haraka haraka, mawili yakipitia kwa Nsajigwa.
    Bao la pili la Simba lilitokana na penalti, baada ya Nsajigwa Shadrack kumkwatua Okwi kwenye eneo la hatari na Felix Sunzu akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 56.
    Okwi alifunga bao la tatu dakika ya 62, baada ya kumtoka Nsajigwa Fusso na kumchambua kipa Said Mohamed Kasarama.
    Baada ya bao hilo, kocha Fred Felix Minziro alipumzishwa Nsajigwa na kumuingiza Godfrey Taita Magina.  
    Dakika ya 67 Uhuru Suleiman aliangushwa na Taita kwenye eneo la hatari na Juma Kaseja akaenda kufunga bao la nne kwa penalti. Patrick Mafisango (sasa marehemu) alifunga bao la tano kwa penalti pia dakika ya 72.
    Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
    Yanga: Yaw Berko/Said Mohamed, Nsajigwa Shadrack/Godfrey Taita, Oscar Joshua, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape/Kenneth Asamoah, Rashid Gumbo na Hamisi Kiiza.
    Naam, hivi ndivyo mambo yalivyokuwa Mei 6, 2012 na baada ya hapo Yanga wakafanya mabadiliko makubwa ya uongozi, wakimtoa Mwenyekiti wao wa wakati huo, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na kuweka safu mpya ya uongozi, chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji, ambaye alianza na sare ya 1-1 Oktoba 3, mwaka jana dhidi ya watani.
    Je, Jumamosi tutarajie nini Uwanja wa Taifa, miamba hiyo ikikutana tena? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. 
    Okwiii...kama Messi siku hiyo

    VIPIGO VINGINE VYA ‘MBWA MWIZI’ SIMBA WALIVYOICHAPA YANGA:

    LIGI KUU BARA:
    JULAI 19, 1977
    Simba v Yanga
    6-0
    WAFUNGAJI:
    Abdallah Kibadeni dk. 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' dk. 60 na 73, Selemani Sanga alijifunga dk. 20.
    JULAI 2, 1994
    Simba v Yanga
    4-1
    WAFUNGAJI:
    Simba: George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani, Dua Saidi Yanga; Constantine Kimanda.
    MACHI 31, 2002.
    Simba Vs Yanga 4-1 (Kombe la Tusker)
    WAFUNGAJI:
    SIMBA: Mark Sirengo dk. 3 na 76, Madaraka Selemani dk. 32 na Emanuel Gabriel dk. 83.
    YANGA: Sekilojo Chambua dk 16.
    (Mechi hii ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Mwamuzi wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, FAT).
    MEI 6, 2012
    Samba 5-0 Yanga SC
    WAFUNGAJI: 
    Emmanuel Okwi (dk 2 na 62), Felix Sunzu (penalti 56), Juma Kaseja (penalti dk 67) na Patrick Mafisango (penalti dk 72)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA NA JINAMIZI LA 5-0 MEI 6 MWAKA JANA TAIFA, MANJI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top