• HABARI MPYA

    Wednesday, May 01, 2013

    HADI LINI ZFA ITAENELEA KUWA GARASA LA TFF?


    KATIKATI ya mwezi Machi  niliandika uchambuzi katika blogu hii uliokuwa ukielezea namna nisivyoridhishwa na utaratibu wa makocha wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, kuteua wachezaji wa kuichezea timu hiyo.
    Nilisema ni jambo la nadra sana, kwa makocha wanaoajiriwa kuifundisha timu hiyo, kuitupia macho ligi kuu au za madaraja mengine hapa Zanzibar kwa ajili ya kutafuta wachezaji wenye uwezo wa kuwa miongoni mwa nyota wanaounda kikosi hicho.

    Hata pale makocha hao, kuanzia Marcio Maximo hadi Kim Poulsen wa sasa, wanapopata nafasi ya kufanya ziara hapa visiwani kuangalia ligi zetu, hatujawahi kuona wakiwaita wachezaji wanaocheza ligi za hapa ingawa mara kadhaa wamekuwa wakisifu kwamba Zanzibar kuna vipaji.
    Japokuwa wapo wanasoka wazuri wanaopata bahati ya kuitwa kwenye timu hiyo, lakini hao ni wale wanaosajiliwa kuichezea ligi kuu Tanzania Bara.
    Imekuwa vigumu sana kusikia makocha wanaoajiriwa kuifundisha Stars, kuchagua wachezaji wanaochezea ligi kuu au za madaraja mengine hapa Zanzibar.
    Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka jana, Poulsen alifanya ziara hapa Zanzibar na kushuhudia baadhi ya mechi za Kombe la Mapinduzi.
    Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuziangalia mechi hizo, alikiri kuvutiwa na wachezaji kadhaa, na kwa kinywa kipana akasema anafikiria kuwaita kwenye kikosi chake.
    Imekuwa vigumu kwa wachezaji wanaochezea ligi hapa nyumbani, kupata nafasi ya kuteuliwa katika timu ya Taifa, hadi pale wanaposajiliwa na klabu za Tanzania Bara.
    Siwezi kufahamu kwa uhakika sababu ya hali hii, kwani kama hoja ni ligi ya Zanzibar kutokuwa na mvuto na ushindani, sababu inayoegemewa na wengi, huwa ninajiuliza huwaje macho ya klabu mbalimbali zivione vipaji hivyo na kuwatupia ndoana wanandinga hao?
    Si kweli kwamba klabu za Yanga, Simba, Azam, JKT Oljoro, Mtibwa Sugar na nyengine zenye wachezaji kutoka Zanzibar, wamewaona kwenye mashindano ya kimataifa yakiwemo Chalenji au Kombe la Kagame, kwani si wote wanaosajiliwa huko wamewahi kushiriki mashindano hayo iwe na timu ya taifa, Zanzibar Heroes, au klabu zao.
    Hii inaonesha kuwa, klabu hizo zinafanya kazi kwa kuwatuma watu wao kutafuta vipaji hapa nchini kupitia ligi za madaraja mbalimbali, na ndio maana zinaviona na kuvivuta katika klabu zao.
    Sasa, kama klabu zinaweza kuhangaika na kuvigundua vipaji vilivyosheheni hapa Zanzibar, iweje Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linashindwa kuonesha wajibu wake juu ya timu ya taifa, kwa kuwasaka wanasoka wa Zanzibar kwa kuwapa nafasi makocha, ili wachague wale wanaohisi wanafaa?
    Kwani mchezaji mpaka asajiliwe na Yanga, Simba au Azam ndipo kipaji chake kiweze kuonekana?
    Katika kuonesha kutokuzipa umuhimu ligi za Zanzibar, siku ya Jumanne Aprili 23, mwaka huu, kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen, aliunda kikosi cha pili cha Taifa Stars ili kupata wachezaji watakaokuwa wakipandishwa kuchezea timu kubwa.
    Kwa mara nyengine, Poulsen amevifumbia macho vipaji vilivyoko Zanzibar na kuita kundi la wachezaji 30, wanaochezea ligi Tanzania Bara.
    Ingawa kuna wachezaji watatu wa Zanzibar, Seif Abdallah ‘Karihe’, Waziri Salum na Samih Haji Nuhu, lakini mfumo umekuwa ndio ule ule kwani nyota hao wanachezea klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam.
    Mbali na wachezaji kibao wanaochezea ligi za madaraja mbalimbali hapa Zanzibar, lakini hakuna asiyejua kwamba visiwa vyetu vimejaaliwa vijana wenye vipaji walio chini ya miaka 20, ambao wamekuwa wakionekana huko Bara kupitia michezo ya Copa Coca Cola inayofanyika kila mwaka.
    Kwa kuwa mashindano ya Copa Coca Cola mwaka huu yamefanyika hivi karibuni tu, basi nilitarajia kama Poulsen alipata wazo la kuunda timu ya pili, angeweza kuvuna baadhi ya wanandinga waliong’ara katika michuano hiyo, kama alipewa fursa na TFF kuwaangalia.
    Kocha huyo amesema timu hiyo iliyopewa jina la ‘Young Taifa Stars’, ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uliozinduliwa Aprili 4 mwaka huu ukilenga kuendeleza wachezaji.
    Wachezaji walioteuliwa kwenye timu hiyo, ni wale ambao wamepita umri wa kuchezea timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na wakubwa ambao hawajapata fursa ya kuingia Taifa Stars, ambapo kocha amesema ataitumia kuangalia uwezo wao.
    Kwa upande mwengine, katika hili, napata mashaka na ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kama angalau kunapokuwa na jambo kama hili, chama chetu cha Zanzibar kinaarifiwa ili nacho kiwatumie makocha wake wazoefu kupendekeza wachezaji wanaofaa kuchezea Taifa Stars.
    Nakumbuka wakati Fulani mwanzoni mwa mwaka jana kabla Ali Ferej hajajiuzulu urais wa ZFA, uongozi wa TFF chini ya Rais wake Leodgar Tenga, ulifika Zanzibar kwa kile kilichoelezwa kuja kuzungumza na wenzao na kuna wapi wanapokosana ili wafungue ukurasa mpya wa ushirikiano.
    Mazungumzo yalifanywa, watu wakanywa soda na kahawa na kumaliza kwa vicheko, lakini tangu hapo hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa kuonesha kuwa uhusiano kati ya pande mbili hizo umeimarika kuliko ulivyokuwa hapo nyuma.
    Tunachokiona zaidi ni kuzidi kwa dharau za TFF kwa ZFA, pamoja na utengano ambao kimsingi usingepaswa kuwepo kwa kuwa tunaambiwa TFF ni mwamvuli unaobeba uwakilishi wa Zanzibar kwenye medani ya kimataifa.
    Nionavyo mimi, ZFA mbele ya TFF ni garasa tu lisiloongeza hesabu kwenye mchezo wa karata, na hali hii itaendelea mpaka labda katiba mpya inayotarajiwa kupatikana, iipe Zanzibar mamlaka kamili ya kuiwakilisha kitaifa na kimataifa katika shughuli za michezo.
    Hili la uteuzi wa wachezaji wa Taifa Stars ni moja kati ya mengi yanayooneesha kuwa ZFA haina kauli mbele ya TFF, nikikumbuka mwanzoni mwa mwaka huu chama chetu kilijipiga kifua kuwafungia wachezaji wa Zanzibar Heroes ambao walikataa kurejesha mgao wa fedha za zawadi walizopata Uganda kwenye michuano ya Chalenji.
    Pamoja na majigambo yake kwamba wachezaji hao Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na wenzake kadhaa hawatakiwi kucheza soka ndani na nje kwa mwaka mmoja, bado tunawaona na kuwasikia wakisakata kabumbu, na TFF imetia pamba masikioni.
    Ni vyema ZFA ijitambue kwamba ni nani na miopama yake mbele ya TFF inaishia wapi.
    Tukae tusubiri majaaliwa yetu ndani ya katiba mpya, labda itatupendelea kujivua mbeleko ya TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HADI LINI ZFA ITAENELEA KUWA GARASA LA TFF? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top