• HABARI MPYA

  Jumapili, Juni 25, 2017

  HALMASHAURI YATENGUA UAMUZI WA KUMPA WANYAMA MTAA DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  HALMASHAURI ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam imetengua mpango wa kuuita Victor Wanyama uliokuwa mtaa wa Viwandani, eneo la Shekilango, Dar es Salaam.
  Taarifa ya Manispaa ya Ubungo leo imesema kwamba, imechukua hatua hiyo kwa sababu jambo hilo lilifanyika kinyume cha utaratibu.
  “Majina ya mitaa hupendekezwa na kamati za mitaa husika kisha hupelekwa kwenye vikao vya WDC vya kata halafu maamuzi ya WDC hupelekwa kwa Mkurugenzi kwa ajili ya kuingizwa kwenye kikao Cha kamati ya Fedha na uongozi, Baraza la Madiwani,”.
  “Halafu DCC,  RCC na Kisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na baadaye kwa Mchapaji mkuu wa serikali na mwisho hutokea kwenye Tangazo la serikali GN. 
  Jamaa akiwa ameng'oa bango la Mtaa wa Victor Wanyama siku moja tu baada ya kuwekwa

  Na hapo ndipp mtaa hujulikana huo ni mtaa fulani. Taratibu za kubadili pia lazima zifuate hatua hizo muhimu,” imesema taarifa hiyo.
  Hatua hiyo inachukuliwa siko moja tu baada ya kiungo kimataifa wa Kenya, Victor Mugubi Wanyama anayechezea Tottenham Hotspur ya England kupewa heshima hiyo kwa Mtaa wa Viwandani uliopo kata ya Shekilango, Manispaa ya Ubungo kupewa jina lake.
  Na hiyo ilifuatia ziara ya kiungo huyo wa klabu ya Tottenham Hotspur ya England nchini kwenye Uwanja wa Kinesi, uliopo eneo hilo kushuhudia mechi za mashindano madogo.
  Kihistoria, Wanyama aliyezaliwa Juni 25, mwaka 1991 alisoma shule ya Kamukunji  na kisoka aliibukia akademi ya JMJ kwao, kabla ya kuchezea klabu za Nairobi City Stars na AFC Leopards katika Ligi Kuu ya Kenya.
  Mwaka 2007 alijiunga na Allsvenskan ya Helsingborg nchini Sweden, lakini akalazimika kuondoka baada ya kaka yake, McDonald Mariga kwenda Parma ya Italia mwaka 2008 na Wanyama akarejea Kenya.
  Baadaye akaenda kufanya majaribio Beerschot AC ya Ubelgiji na kufuzu, hivyo kusaini mkataba wa miaka wa minne kuanza kucheza rasmi Ulaya mwaka 2008, kabla ya mwaka 2011 kununuliwa na Celtic ya Ligi Kuu ya Scotland.
  Victor Wanyama jana baada ya kuambiwa Mtaa wa Viwanjani umepewa jina lake alifurahi sana

  Mwaka 2013 alinunuliwa na Southampton ya England kwa dau la Pauni Milioni 12.5 na kuwa Mkenya wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England. Baada ya mechi 85 akifunga mabao manne, Wanyama akanunuliwa na Tottenham Hotspur mwaka jana kwa dau la Pauni Milioni 11 na msimu huu ameiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, nyuma ya Chelsea walioibuka mabingwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HALMASHAURI YATENGUA UAMUZI WA KUMPA WANYAMA MTAA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top