• HABARI MPYA

  Jumapili, Juni 25, 2017

  WAMECHOMA MOTO JEZI YA YANGA, SIYO YA HARUNA

  WIKI hii klabu ya Yanga imeamua kuachana na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima baada ya kutofikia makubaliano naye juu ya mkataba mpya.
  Katibu wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa alithibitisha kuachana na Niyonzima vizuri tu baada ya mazungumzo baina yao kutofikia mwafaka wa mkataba mpya.
  “Hata hivyo Haruna Niyonzima bado ana mkataba mpaka mwezi Julai na Yanga Sc, lakini hatutaweza kuendelea kuwa nae kwa msimu ujao kwani hatukuweza kufikia mwafaka katika mazungumzo yetu na yeye licha ya timu yetu kuwa na nia za kuendelea naye kwa misimu miwili ijayo,”alisema.
  Awali, Niyonzima alikaririwa na Bin Zubeiry Sports – Online akisema kwamba yuko kwenye mazungumzo na Yanga juu ya mkataba mpya na wakati huo huo Simba nao wanamuhitaji.
  Na tayari inaelezwa Haruna amesaini Simba, ingawa yeye mwenyewe kila anapotafuta amekuwa hapatikani kwenye simu yake.
  Mzaliwa huyo wa Gisenyi, Rwanda Februari 5, mwaka 1990 alijiunga na Yanga SC mwaka 2011, akitokea APR ya Rwanda aliyoanza kuichezea mwaka 2007 baada ya kujiunga nayo kutoka Rayon Sport iliyomsajili mwaka 2006 kutoka Etincelles iliyomuibua kisoka nchini humo.
  Wakati Haruna anaondoka, inaelezwa mshambuliaji mwingine aliyechezea timu hiyo kwa misimu miwili iliyopita, Donald Ngoma naye anaweza kuondoka.
  Ngoma inasemekana ametaka fedha nyingi, ambazo Yanga hawana uwezo wa kutoa kwa sasa, hivyo mahasimu, Simba wameahidi kumpa na anaweza kuhamia Msimbazi.
  Bahati nzuri, wachezaji wengine tegemeo kama Mrundi, Amissi Tambwe, Mzambia, Obrey Chirwa na wazalendo kama Hassan Kessy, Juma Abdul, Geoffrey Mwashiuya na Simon Msuva wana mikataba.
  Lakini Yanga wanakabiliwa na jakamoyo pia juu ya kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko ambaye naye amemaliza mkataba na haijulikani watamalizana vipi.
  Pamoja na hayo, Yanga nao wamejitahidi kusajili wachezaji kadhaa japo hadi sasa imewatambulisha wawili tu, beki Abdallah Hajji ‘Ninja’ kutoka Taifa Jang’ombe na kiungo Emmanuel Buswita kutoka Mbao FC kwa sababu wengine iliyowasaini hawajamaliza rasmi mikataba na klabu zao.
  Msimu uliomalizika Yanga ilitozwa faini ya Sh. Milioni 50 tu kwa kumsajili Hassan Kessy kutoka Simba akiwa amebakiza wiki moja na Mkwasa amesema chini yake kama Katibu hataki kosa hilo lijitokeze.
  Na habari zisizo rasmi zinasema, Yanga imewasajili pia, kipa Mcameroon, Youthe Rostand kutoka African Lyon, beki Babu Ally Seif kutoka Kagera Sugar na mshambuliaji Ibrahim Hajib kutoka kwa mahasimu Simba.
  Na bado wapo wengine wanatajwa kuwa mbioni kusaini kwa wana Jangwani hao, wakiwemo viungo Mudathir Yahya kutoka Azam, Raphael Daudi kutoka Mbeya City na mshambuliaji Stahmili Mbonde kutoka Mtibwa Sugar.
  Lakini usajili wa Simba ndiyo umekuwa wa kusisimua zaidi katika dirisha hili, kutokana na kuchukuwa wachezaji wengi wenye majina makubwa.
  Mbali na Haruna Niyonzima na Donald Ngoma ambao Simba haijathibitisha kuwa na mpango nao ingawa huo ndiyo ukweli, lakini Wekundu hao wa Msimbazi wamechukua nyota watatu Azam FC, kipa Aishi Manula, beki Shomary Kapombe na mshambuliaji John Bocco.   
  Simba imewasajili pia kipa Emmanuel Mseja, mabeki Jamal Mwambeleko kutoka wote Mbao FC, Ally Shomary kutoka Mtibwa Sugar na Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans, huku pia mshambuliaji wake wa zamani, Emmanuel Okwi aliwasili jana tayari kusaini mkataba kurejea Msimbazi.
  Usajili huo na pamoja na mpango wa kuwasajili Haruna na Ngoma – basi wana Simba wamekuwa na furaha sana na kwa ujumla wanatamba katika soko la usajili.
  Wapo mashabiki wa Yanga wanamchukulia Haruna kama msaliti baada ya kuondoka Yanga, lakini wanasahau hata alipokuja nchini alivutiwa na fedha alizopelekewa na Abdallah Bin Kleb. Kule Kigali.
  Kama kuna hisani zozote Bin Kleb alimfanyia Haruna ikiwemo kumtibu mama yake mzazi India kama inavyoelezwa, alifanya hivyo kwa sababu alikuwa mchezaji wa Yanga na tayari walikuwa marafiki.
  Linapokuja suala la kazi, kinachotazamwa ni maslahi – na Haruna amekuwa jasiri kwa kufanya maamuzi magumu, kuondoka katika klabu aliyochezea kwa muda mrefu na kutengeneza marafiki kama Bin Kleb.
  Wapo watu walichoma jezi ya Yanga yenye jina la Haruna kuonyesha hisia zao za kuchukia kuhama kwake.
  Hawakuchoma jezi ya Haruna, wamechoma moto jezi ya Yanga. Jezi ya Haruna ni moja tu, ni ile ya timu ya taifa ya Rwanda, hizi za klabu anaweza akavaa hata tatu kwa mwaka mmoja.
  Mei 20, mwaka huu aliichezea Yanga ikifungwa 1-0 na Mbao FC mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pale CCM Kirumba, Mwaza na tunatarajia Agosti ataanza kuichezea Simba – lakini Rwanda hatahama, hivyo Yanga wajue wamechoma moto jezi yao wenyewe, si ya Haruna. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAMECHOMA MOTO JEZI YA YANGA, SIYO YA HARUNA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top