• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 19, 2017

  NIYONZIMA: MIMI BADO MCHEZAJI WA YANGA, SIJASAINI SIMBA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, amesema yeye bado ni mchezaji wa Yanga na hajasaini kwa mahasimu Simba kama inavyovumishwa.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mchana, Niyonzima amesema kwamba anastaajabishwa na uvumi kwamba yeye amesaini Simba, wakati si kweli.
  Pamoja na hayo, Niyonzima amekiri kufanya mazungumzo na viongozi wa Simba, lakini hajafikia hata makubaliano ya kusaini zaidi ya kuwasikiliza tu na ofa yao.
  Haruna Niyonzima amesema yeye bado ni mchezaji wa Yanga na hajasaini kwa mahasimu Simba kama inavyovumishwa

  “Nipo kwenye likizo, nimeelekeza fikra zangu kwenye mambo ya familia zaidi kwa kipindi hiki, pili mimi naamini kama ningekuwa nimesaini huko (Simba), au nimesaini huku (Yanga) kila mtu angejua, hivyo kwa sasa sijasaini timu yoyote,”amesema.
  Haruna amesema kwa sasa anasikiliza ofa mbalimbali zinazoletwa kwake, kabla ya kuamua asaini wapi. “Mimi kama mfanyabiashara naweza nikaongea na timu yoyote, haya yanayoendelea sasa yataisha,”amesema.
  Mzaliwa huyo wa Gisenyi, Rwanda Februari 5, mwaka 1990 alijiunga na Yanga SC mwaka 2011, akitokea APR ya Rwanda aliyoanza kuichezea mwaka 2007 baada ya kujiunga nayo kutoka Rayon Sport iliyomsajili mwaka 2006 kutoka Etincelles iliyomuibua kisoka nchini humo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NIYONZIMA: MIMI BADO MCHEZAJI WA YANGA, SIJASAINI SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top