• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 22, 2017

  LWANDAMINA: AFRIKA INA VIPAJI VINGI, NITAMPATA MBADALA WA NIYONZIMA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina amesema kwamba Afrika ina vipaji vingi anaamini atapata mbadala wa kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima anayehamia kwa mahasimu, Simba SC.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Zaambia, Lwandamina amesema kwamba ingawa hajathibitisha kama kweli Niyonzima anakwenda Simba, lakini anaamini mbadala wake atapatikana.
  “Mbadala wake anaweza kupatikana na Afrika haiwezi kukosa vipaji. Wakati mwingine familia zinaondokewa na mtu hadi unaanza kufikiria bila fulani mambo hayawezi kwenda,”amesema.
  Lakini Lwandamina ameonyesha kushitushwa kidogo na tetesi za mshambuliaji wake, Mzimbabwe Donald Ngoma naye kuwa mbioni kujiunga na Simba.
  George Lwandamina amesema atapata mbadala wa Haruna Niyonzima anayehamia kwa mahasimu, Simba SC

  Yanga jana, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Charles Boniface Mkwasa imethibitisha kuachana na Nahodha wa Rwanda, Niyonzima baada ya miaka sita na taarifa zinasema anakwenda Simba, lakini pia tetesi zinasema Ngoma naye yuko njia hiyo.
  Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia amesema mapema aliagiza wasajiliwe wachezaji watano muhimu, ambao ni beki wa kushoto, beki wa kati, kiungo wa ulinzi, winga wa kushoto na mshambuliaji baada ya kuona mapungufu kikosini msimu uliopita. 
  “Nimeagiza wasajiliwe mshambuliaji wa nguvu, mfungaji wa magoli, mwenye maamuzi ya haraka, mwenye kujiamini na mpira, anayeweza kutumia miguu yote. Pia kiungo mkabaji, beki wa kati anayetumia miguu yote, kiungo wa kushoto na beki wa kushoto,”amesema.
  Mwalimu huyo wa zamani wa Zesco United ya kwao, Lwandamina amesema hakutaja jina la mchezaji hata mmoja, bali alitaja sifa za wachezaji wa kusajiliwa na kwa sababu Katibu Mkwasa ni kocha kitaaluma, anaamini zoezi hilo litakwenda vizuri. 
  Amesema yeye anatarajiwa kurejea nchini wiki ya kwanza ya Julai kuanza maandalizi ya msimu mpya. Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka jana kuchukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm baada ya mafanikio yake Zesco akiifikisha Nusu Fainali mwaka jana.
  Ameisaidia Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika msimu mgumu, ambao klabu ilikuwa inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi iliyosababisha migomo ya mara kwa mara ya wachezaji. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: LWANDAMINA: AFRIKA INA VIPAJI VINGI, NITAMPATA MBADALA WA NIYONZIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top