• HABARI MPYA

    Wednesday, June 21, 2017

    RAIS MAGUFULI AWAPA POLE YANGA MSIBA WA ‘ALLY MASIZI’

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amewapa pole Yanga SC kufuatia msiba wa aliyekuwa mwanachama na shabiki wa klabu hiyo, Ally Mohammed ‘Ally Yanga’.
    Ally Yanga alifariki dunia jana baada ya ajali ya gari iliyotokea, eneo la Mpwapwa, Dodoma.
    Taarifa zinasema Ally Yanga alikuwa kwenye msafara wa mbio za Mwenge kabla ya kupata ajali hiyo barabara ya Wiyenzele kuelekea Chipogoro na kufariki hapo hapo.
    Enzi za uhai wake, Ally alikuwa maarufu kwa staili ya kushabikia akiwa amejipaka masizi usoni huku ameweka matambara tumboni kutengeneza kitambi. Na majina yake mengine ya utani yalikuwa Ally Masizi na Ally Tumbo Tumbo, mbali ya Ally Yanga. 
    Rais Dk. John Pombe Magufuli amewapa pole Yanga SC kufuatia msiba wa aliyekuwa mwanachama na shabiki wa klabu hiyo, Ally Mohammed ‘Ally Yanga’ (picha ndogo juu kulia)

    Mwili wa marehemu umepelekwa nyumbani kwao, Shinyanga ambako ndiko msiba ulipo, Stendi ya zamani na mazishi yanatarajiwa kufanyika leo.
    Ally aliyezaliwa mkoani Shinyanga Machi 1, mwaka 1984 katika familia ya watoto sita, kabla ya umauti wake inafahamika alikuwa anaishi Yombo Vituka, Dar es Salaam.
    Aliibukia Ubungo miaka ya nyuma kidogo ambako alikuwa anafanya shughuli ya kusajili laini za simu za mkononi katika vibanda vilivyokuwa pembeni ya kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, Ubungo Terminal.
    Na alianza kuonekana Uwanja wa Taifa pamoja na kikundi cha mashabiki wa Yanga cha Ubungo Terminal, ambako ndipo lilipokuwa tawi lake.
    Lakini tangu baada ya uchaguzi Mkuu Novemba 2015, Ally Yanga ameadimika viwanja vya soka kutokana na kujikita zaidi kwenye shughuli za Chama cha Mapinduzi CCM.
    Ally hakuwa shabiki wa Yanga tu, enzi za uhai wake alikuwa akizishabiki pia timu za taifa, kuanzia za vijana na wakubwa za wanawake na wanaume. 
    Alikuwa maarufu Afrika Mashariki kutokana na kwenda kuishabikia Taifa Stars kwenye mechi za Kombe la CECAFA Challenge nchi za Kenya na Uganda. Lakini pia amewahi kusafiri hadi nje ya Afrika ya Afrika Mashariki akiwa na Taifa Stars kwenye mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe ka Dunia. Mungu ampumzishe kwa amani Ally Yanga. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MAGUFULI AWAPA POLE YANGA MSIBA WA ‘ALLY MASIZI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top