• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 20, 2017

  ABDI BANDA AWAKAMUA SIMBA SH MILIONI 65

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda amesema kwamba amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba SC kwa dau la Sh. Milioni 65, lakini kuna kipengele akipata timu auzwe wakati wowote.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo asubuhi kwenye mazoezi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa na michuano ya COSAFA Castle nchini Afrika Kusini baadaye mwezi huu, Banda amesema kwamba wakati wowote, Meneja wake Abdul Bosnia atafika Dar es Salaam ili wasaini mkataba huo mpya na Simba.
  Ukuta wa Taifa Stars; Abdi Banda wa pili kushoto akiwa na mabeki wenzake wa timu ya taifa, kutoka kulia Salim Mbonde, Shomary Kapombe na Gardiel Michael (kushoto)
  “Mimi mkataba wangu zimebaki siku tano umalizike, lakini naweza nikaendelea nao (Simba) nikasaini ndani ya siku mbili hizi au nikirudi kutoka Afrika Kusini,”amesema Banda.
  Beki huyo wa zamani wa Coastal Union ya Tanga, amesema kwamba alikwishafanya mazungumzo na uongozi wa Simba na kukubaliana dau la Sh. Milioni 65 kusaini miaka miwili mbali na mshahara wake ambao ameufanya siri.
  “Dau langu wenyewe wanajua na nilishawaambia nataka Milioni 65 na tulikwishaelewana kila kitu hadi mshahara, nahisi kitu kinachochelewesha ni meneja wangu yupo safarini, siku si nyingi atarudi na kila kitu kitakuwa sawa,”amesema.
  Banda yumo kwenye kikosi cha Taifa Stars, kinachotarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) Castle nchini Afrika Kusini kuanzia Juni 25, mwaka huu.
  Taifa Stars iliyoweka kambi hoteli ya Urban Rose iliyopo iliyopo eneo la Kisutu, huku ikifanya mazoei Uwanja wa JMK Youth Centre, inatarajiwa kuondoka nchini Juni 22 kwenda Afrika Kusini kushiriki michuano ya COSAFA kama wa waalikwa kwa mwaka wa pili mfululizo na mara ya tatu kwa ujumla kihistoria. 
  Tanzania imepangwa kundi A pamoja na Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B lina timu za Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe – na Botswana, Zambia, Namibia, Lesotho na Swaziland na wenyeji, Afrika Kusini zitacheza mechi maalumu za mchujo kuwania kuingia robo fainali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ABDI BANDA AWAKAMUA SIMBA SH MILIONI 65 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top