• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 23, 2017

  HIMID MAO: YANGA NILIWACHOMOLEA KITAMBO, HAKUNA HIYO ISHU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa kimataifa nchini, Himid Mao Mkami amesema habari za yeye kwenda kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC ni uzushi tu.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana kabla ya kwenda Afrika Kusini na timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya COSAFA, Mao amesema kwamba ni kweli Yanga walimtafuta, lakini hakuwakubalia.
  “Ni kweli kwamba Yanga walinitafuta, lakini nikawaambia tu wazi nina mkataba na Azam na pia nina mipango yangu tofauti na kuendelea kucheza Tanzania,”alisema Himid.
  Himid Mao (kushoto) amesema habari za yeye kwenda Yanga SC ni uzushi mtupu

  Nahodha huyo Msaidizi wa Taifa Stars ambaye ataiongoza timu kwenye michuano ya COSAFA kufuatia kutokuwepo kwa Nahodha Mkuu, Mbwana Samatta amesema kwamba malengo yake makubwa kwa sasa ni kutoka nje.
  “Hapa nilipo nina ofa kama sita au saba za timu za nje zinazonitaka na kwa sasa wakala wangu anashughulikia hilo suala. Na ni vizuri hata klabu yangu imeridhia sana mpango wa kwenda nje,”amesema.
  Himid amesema kwa ujumla wazo la kwenda nje lina msukumo mkubwa kuanzia kwenye familia yake hadi wazazi nao wanapenda kumuona akiondoka nchini. “Hata mke wangu hataki nibaki hapa, na mzee Mao naye pia anataka niondoke,”amesema.
  Mapema Mei Himid alikwenda Denmark kufanya majaribio ya kujiunga Randers FC ya Ligi Kuu ya nchini humo, inayofundishwa na kocha Olafur Kristjsnsson na ikaripotiwa alifuzu.
  Ilitarajiwa Randers kuingia kwenye mazungumzo na Azam FC juu ya biashara ya mchezaji huyo, aliyezaliwa Novemba 5, mwaka 1992 Dar es Salaam, lakini hadi sasa bado kimya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HIMID MAO: YANGA NILIWACHOMOLEA KITAMBO, HAKUNA HIYO ISHU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top