• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 30, 2017

  KAMATI YA UTENDAJI SIMBA SC KUJADILI MUSTAKABALI WA KLABU KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Utendaji ya Simba SC kesho inatarajiwa kukutana kujadili mustakabali wa klabu baada ya viongozi wake wakuu, Rais Evans Elieza Aveva na Geoffrey Hiriki Nyange ‘Kaburu’ kuwekwa rumande kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo utakatishaji wa fedha
  Taarifa ya klabu kwa vyombo vya Habari leo, imesema Kamati ya Utendaji ya klabu itakutana pamoja na mambo mengine kuangalia masuala muhimu ya uendeshaji wa klabu katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  “Tunaamini Kamati ya Utendaji itakuja na majawabu sahihi ya kuhakikisha shughuli za klabu zinaendelea kama kawaida,”imesema taarifa hiyo.
  Rais wa Simba, Evans Elieza Aveva (kulia) akiwa na Mjumbe wa kuteuliwa, Zacharia Hans Poppe (kushoto) 
  Taarifa imesema klabu imesikitishwa na kukamatwa kwa viongozi hao na inaungana na wanachama, wapenzi na mashabiki wake katika kipindi hiki kigumu ambacho viongozi wao wakuu wanashikiliwa na vyombo vya Dola na wamenyimwa dhamana. 
  “Klabu kwa sasa imeandaa jopo la mawakili litakalowatetea viongozi wetu na tunaamini Mahakama itatenda haki pande zote zinazohusika na shauri hilo. Tunawaomba Watanzania, wapenzi na mashabiki wetu wawe watulivu wakisubiri taarifa rasmi ya kikao cha Kamati ya Utendaji,”imesema taarifa hiyo.
  Baada ya kukosekana kwa Aveva na Kaburu, wanaobaki ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji tu, wa kuchaguliwa na kuteuliwa. Wajumbe wa kuchaguliwa ni Collins Frisch, Said Tuliy, Ally Suru, Iddi Kajuna na Jasmine Costa wakati wa kuteuliwa ni Zacharia Hans Poppe, Salim Abdallah ‘Try Again’, Mohammed Nassor, Kassim Dewji, Musley Ruweih. 
  Aveva na Makamu wake, Kaburu jana walipelekwa mahabusu hadi Julai 13, mwaka huu baada ya kunyimwa dhamana kufuatia kusomewa mashitaka matano Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
  Wawili hao walifikishwa mahakamani mapema asubuhi na kusomewa mashitaka hayo matano mchana, ambayo ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodai kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni Rais Aveva na Makamu wake, Kaburu kiasi cha dola za Kimarekani 300,000.
  Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwenye benki ya CRDB tawi la Azikiwe mjini Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sharia, ambapo inadaiwa Rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
  Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka kwenye benki ya  Barclays tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu aliyemsadia Aveva kutakatisha fedha katika Barclays baada ya kughushi nyaraka.
  Baada ya kusomewa mashitaka hayo na wakili wa Serikali, Christopher Msigwa, washitakiwa hao walikana mashitaka yote na kupelekwa rumande hadi Julai 13, mwaka huu huku wakinyimwa dhamana.
  Wawili hao walipandishwa kizimbani jana baada ya juzi kukamatwa na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uchunguzi juu ya tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutokana na mchezaji Emmanuel Okwi.
  Inadaiwa kuna ‘ufisadi’katika mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi kwenda klabu ya Esperance ya Tunisia dili ambalo liliripotiwa kugharimu dola za Kimarekani 300,000, zaidi ya Sh. Milioni 600 za Tanzania.
  Lakini Aveva hakuwapo madarakani wakati Simba inamuuza Okwi mwaka 2013, bali Kaburu alikuwa Makamu wa Rais, chini ya Rais wa wakati huo, Alhaj Ismail Aden Rage.
  Hata hivyo, Esperance ilichelewa kulipa fedha hizo na hadi Machi mwaka jana, wakati huo tayari Aveva ni Rais wa klabu na Kaburu ni Makamu wake, baada ya Rage kutogombea tena.
  Okwi alinunuliwa na Etoile Januari mwaka 2013, miaka mitatu tu baada ya kujiunga na Simba mwaka 2010, lakini baada ya miezi mitatu akatofautiana na klabu ya Tunisia kufuatia na kufungua kesi FIFA akiomba aruhusiwe kucheza klabu nyingine kulinda kipaji chake wakati mgogoro wake na Etoile unaendelea.
  Etoile ilisitisha huduma kwa Okwi, baada ya kukerwa na desturi ya mchezaji huyo kuchelewa kurejea kujiunga na timu kila alipokuwa anaporuhusiwa kwenda kujiunga na timu yake ya taifa Uganda.
  Akasaini tena SC Villa katikati ya mwaka 2013 kabla ya Desemba mwaka huo, kuhamia Yanga SC- wakati wote huo kesi yake na Etoile ikiendelea FIFA na Simba walikuwa hawajalipwa fedha zao.
  Simba nayo ilifungua kesi FIFA ikisistiza kulipwa fedha zake baada ya kumuuza mchezaji huyo Etoile Januari 2013.
  Okwi na Simba wakaungana tena mwaka 2014 baada ya mchezaji huyo kutofautiana na Yanga pia, akidai ilishindwa kummalizia fedha zake za usajili, hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumruhusu kuondoka, naye akarejea Msimbazi.
  Kabla haijapata fedha za kumuuza Okwi Etoile, Simba ikamuuza tena Okwi klabu ya Sonderjyske ya Denmark kwa dau la  dola za Kimarekani 110,000 zaidi ya Sh. Milioni 230 za Tanzania.
  Hata hivyo, Denmark nako aliposaini mkataba wa miaka mitano, aliondoka baada ya miaka miwili tu na kurejea SC Villa mapema mwaka huu, kabla ya juzi kusaini mkataba wa miaka miwili kujiunga tena na Simba kwa mara ya tatu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAMATI YA UTENDAJI SIMBA SC KUJADILI MUSTAKABALI WA KLABU KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top