• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 21, 2017

  MANULA: MIMI NA SIMBA SAFI, TUNASUBIRI MUDA TU

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KIPA namba moja nchini, Aishi Salum Manula amevunja ukimya baada ya kusema wazi tayari yeye ni mchezaji mpya wa Simba SC.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini Dar es Salaam, Aishi alisema kwamba amekwishafikia makubaliano na uongozi wa Simba kujiunga na klabu yao kwa miaka miwili ijayo na kwa sasa anasubiri amalize mkataba wake Azam Julai 30 ili ahamie rasmi Msimbazi.
  “Bado sijasaini Simba, mimi bado ni mchezaji wa Azam FC ila nimekwishafanya mazungumzo na Simba tumekubaliana, nasubiri mkataba wangu uishe Azam ndiyo tumalize makubaliano na Simba,” alisema Manula.
  Aishi Salum Manula amevunja ukimya baada ya kusema wazi tayari yeye ni mchezaji mpya wa Simba SC

  Manula anatua Simba kwa dau la Sh. Milioni 50 kwa miaka miwili na atakuwa analipwa Milioni 3 kwa mwezi mshahara.
  Hata hivyo, mkataba huo unasema, Aishi atalipwa kwa awamu fedha hizo, Sh. Milioni 25 wakati wa kusiani, Milioni 5 kabla ya Agosti 30 na Sh. Milioni 20 atamaliziwa kabla ya Desemba mwaka huu.
  Aishi anakuwa mchezaji wa tatu tegemeo wa Azam FC kuhamia Simba SC, baada ya beki Shomary Kapombe na aliyekuwa Nahodha wa timu hiyo ya Chamazi, John Raphael Bocco kutangulia pia Msimbazi.
  Wachezaji wote wanaondoka Azam FC wakati mikataba yao inamalizika mwishoni mwa mwezi huu na mazungumzo ya kusaini mikataba mipya yalishindikana, kutokana na sera mpya za timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kutotumia fedha nyingi katika kusajili.
  Aishi aliyesimama langoni jana katika lango la timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ikilazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho katika mchezo wa kwanza wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 aliibukia kwenye timu ya vijana ya Azam FC mwaka 2013.
  Na baada ya kupandishwa kikosi cha kwanza chini ya kocha wa wakati huo, Muingereza Stewart Hall haikuchukua muda mrefu kuwa kipa wa kwanza akimpindua Mwadini Ali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MANULA: MIMI NA SIMBA SAFI, TUNASUBIRI MUDA TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top