• HABARI MPYA

  Thursday, July 13, 2017

  ROONEY AREJEA NA MABAO EVERTON WAKIIKALISHA GOR MAHIA ‘KWA MCHINA’

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Wayne Rooney amekuwa na mwanzo mzuri akiichezea kwa mara ya kwanza klabu yake, Everton baada ya kufunga katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam maarufu kama Kwa Mchina.
  Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, alifunga bao zuri kwa shuti la umbali wa mita 30 dakika ya 34.
  Mchezaji huyo aliyerejea Everton wiki iliyopita baada ya miaka 13 tangu ahamie Manchester United amekumbushia kitu alichofanya wakati anajiunga na timu hiyo ya Merseyside kwa mara ya kwanza kabisa alipofunga bao lake la kwanza katika mechi ya kwanza dhidi ya Arsenal mwaka 2002, siku tano kabla hajatimiza miaka 17.
  Wayne Rooney akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza leo dhidi ya Gor Mohia ya Kenya PICHA ZAIDI GONGA HAPA 

  Leo Rooney alipata mpira akiwa umbali wa mita 40, akauvuta mbele kidogo kabla ya kufumua shuti lililotinga nyavuni.
  Hata hivyo, Gor Mahia wakasawazisha bao hilo kabla ya mapumzkiko kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Rwanda, mzaliwa wa Uganda, Meddie Kagere.
  Kipindi cha pili makocha wote, Dylan Kerr wa Gor Mahia na Ronald Koeman wa Everton wakabadilisha vikosi vyao vyote, lakini bahati ilikwenda kwa timu ya Ligi Kuu ya England, The Toffees waliopata bao la ushindi kupitia kwa Kieran Dowell.
  Gor Mahia ilipata nafasi ya kucheza na Everton baada ya kuibuka bingwa wa michuano ya SportPesa Super Cup, ikiwafunga mahasimu, AFC Leopatrds 3-0.
  Timu nane zilishiriki michuano hiyo ya wiki moja Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam – mbali na Gor na Leopards, nyingine ni Tusker na Nakuru All Stars za Kenya pia, Jang’ombe Boys ya Zanzibar, Simba, Yanga na Singida Unted za Tanzania.
  Wenyeji Simba na Yanga hawakufika mbali kwa sababu wiki ya michuano hiyo wachezaji wao wengi nyota walikuwa kwenye vikosi mbalimbali vya timu za taifa na kujikuta wakitumia wachezaji wengi wa akiba na wa timu za vijana.  
  Vikosi vya leo vilikuwa; 
  Gor Mahia kipindi cha kwanza; Boniface Oluoch, Godfrey Walusimbi, Musa Mohammed, Haron Shakava, Karim Niziyimana, Ernest Wendo, Kenneth Muguna, George Odhiambo, Meddie Kagere, Jacques Tuyisenge na Boniface Omondi.
  Kipindi cha pili: Peter Odhiambo, Innocent Wafula, Mike Simiyu, Wellington Ochieng, Joachim Oluoch, Philemon Otieno, Francis Kahata, Jean Baptiste, Oliver Maloba, Jeconia Uyoga na Timothy Otieno.
  Everton FC kipindi cha kwanza; Stekelenburg; Connolly, Jagielka, Kenny, Williams; Schneiderlin, McCarthy, Lennon, Klaassen, Lookman na Rooney.
  Kipindi  cha pili: Hewelt, Baines, Keane, Davies, Mirallas, Pennington, Calvert-Lewin, Gueye, Barry, Besic na Dowell.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ROONEY AREJEA NA MABAO EVERTON WAKIIKALISHA GOR MAHIA ‘KWA MCHINA’ Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top