• HABARI MPYA

    Saturday, July 08, 2017

    MANULA ‘AMVULIA KOFIA’ SAID MOHAMMED MDUDA KWA KAZI YA JANA

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KIPA namba moja Tanzania, Aishi Salum Manula amempongeza kipa wa pili, Said Mohammed Mduda baada ya jana kuisaidia Taifa Stars kuchukua nafasi ya tatu katika michuano ya COSAFA Castle nchini Afrika Kusini.
    Taifa Stars imechukua nafasi ya tatu Kombe laa COSAFA Castle usiku wa jana baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg na kupitia akaunti yake ya Instagram kipa mpya wa Simba, Manula anayetokea Azam FC amempongeza Mduda.

    Kipa Said Mohammed Mduda jana alipangua penalti ya Nahodha wa Lesotho, Thapelo Mokhehle kuipa Tanzania ushindi wa tatu COSAFA

    “Hakika wewe ni bora kaka, na mara zote umekuwa bora. Kazi uliyoifanya leo ni kubwa mno kwetu Watanzania. Pia unastahili kupewa pongezi kwa ulichofanya. Kwangu mimi wewe ndiye Mchezaji Bora wa Mechi na ulistahili kaka, endelea hivyo hivyo,”alisema Manula jana baada ya mechi.
    Kipa huyo wa Mtibwa Sugar ya Morogoro aliyewahi kudakia Yanga ya Dar es Salaam na Maji Maji ya Songea, alikuwa shujaa jana Taifa Stars baada ya kupangua penalti ya Nahodha wa Mamba, Thapelo Mokhehle kufuatia Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.
    Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao,Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.


    Aishi Manula (kushoto) amempongeza Said Mohammed (kulia) kwa kazi ya jana Kombe la COSAFA Castle 

    Ushindi unakuja siku 25 baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 Juni 10, mwaka huu katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Kutoka na ushindi huo, Tanzania inaondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.
    Fainali ya COSAFA Castle 2017 itachezwa Jumapili Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg baina ya majirani, Zambia na Zimbabwe na bingwa atapata dola 42,000 na mshindi wa pili dola 21,000.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANULA ‘AMVULIA KOFIA’ SAID MOHAMMED MDUDA KWA KAZI YA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top