• HABARI MPYA

    Wednesday, July 05, 2017

    MANJI ASOMEWA MASHITAKA YA UHUJUMU UCHUMI KITANDANI MUHIMBILI, ANYIMWA DHAMANA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji leo amenyimwa dhamana baada ya kusomewa mashitaka ya Uhujumu Uchumi, ikiwamo kukutwa na vitambaa vya sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akiwa amelazwa kitandani katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
    Hiyo ni baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kulazimika kuhamishia shughuli zake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuwasomea mashtaka ya uhujumu uchumi Manji mwenyee umri wa miaka (41) na wenzake.
    Manji na wenzake pia wanatuhumiwa kukutwa na mihuri ya mbalimbali ya JWTZ pasipo na uhalali, vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 236.5.
    Mahakama hiyo ilifika viunga vya taasisi hiyo Saa 9:10 alasiri na moja kwa moja kuingia wadi namba moja alikolazwa Manji huku washtakiwa wenzake wakifikishwa na gari ya polisi aina ya Land Cruiser yenye namba za usajili T 968 DHS na kuungana na mtuhumiwa mwenzao.
    Mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, ilianza kusikiliza mashtaka ya Jamhuri saa 9:35 katika wodi hiyo.
    Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga, Mutalemwa Kishenyi na Tulumanywa Majigo huku, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na Seni Malimi.
    Majigo aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni, Ofisa Rasilimaliwatu Deogratias Kisinda (28), Mtunza Stoo, Abdallah Sangey (46) na Mtunza Stoo msaidizi, Thobias Fwele (430
    Alidai katika shtaka la kwanza kuwa Juni 30, mwaka huu eneo la Chang'ombe Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Manji na wenzake walikutwa na askari polisi wakiwa na Mabunda (majola) 35 ya vitambaa vya vinavyotengezea sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 192.5 na kwamba zilipztikana isivyo halali.
    Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa mekutwa Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A' Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabando nane ya sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 44.
    Upande huo wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa, Juni 30,mwaka huu eneo la tukio la kwanza, washtakiwa walikutwa na mhuri wa JWTZ uliokuwa na maandishi 'Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha Jeshi JWTZ' bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.
    Majigo aliendela kudai katika shtaka la nne, siku ya tukio la tatu, washtakiwa wote kwa pamoja walikuwa na mhuri wenye maandishi "Kamanda Kikosi 834 Kj Makutupora Dodoma" bila uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.
    Shitaka la tano, siku ya tukio la tatu na la nne, mshtakiwa alikutwa na mhuri wenye maandishi "Comanding Officer 835 Kj  Mgambo P.O BOX 224 Korogwe" bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha uslama wa nchi.
    Ilidaiwa katika shtaka la sita, Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A', washtakiwa wote walikutwa na pleti namba za gari zenye usajili wa SU 383 iliyopatikana isivyo halali.
    Majigo alidai katika shtaka la saba, eneo la tukio la sita, washtakiwa walikutwa na pleti namba za gari zenye namba ya usajili SM 8573 iliyopatikana isivyo halali.
    Kwa mujibu wa mashtaka hayo yaliyofunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao.
    Upande wa Jamhuri uliwasilisha hati ya kuzuia dhamana kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), akiomba washtakiwa wasipewe dhamana kwa usalama wao na maslahi ya taifa.
    DPP pia alieleza sababu nyingine kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kushughulikia dhamana dhidi ya kesi hiyo.
    Hata hivyo, upande wa utetezi ulidai kuwa upande wa Jamhuri una nia mbaya kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya washtakiwa kuwasilisha hati hiyo ni kuwanyima haki.
    Hakimu Shaidi alisema upande wa utetezi wawasilishe hoja zao Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kusikiliza kesi yao na kwamba hawezi kutoa amri yoyote chini ya mahakama yake.
    Alisema kesi hiyo itatajwa Julai 19, mwaka huu na washtakiwa watatu walipelekwa mahabusu ya Keko huku Manji akiwa chini ya ulinzi wa polisi wodini hapo wakati akisubiri askari magereza kupokea hati yake ya kuwa mahabusu.
    Mahakama hiyo ilimaliza shughuli zake saa 10.35 alasiri na wakati wote Manji alikuwa amelala kitandani huku washtakiwa wenzake wakiwa wamesimama wakati mashtaka yanasomwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI ASOMEWA MASHITAKA YA UHUJUMU UCHUMI KITANDANI MUHIMBILI, ANYIMWA DHAMANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top