• HABARI MPYA

  Wednesday, July 12, 2017

  BANDA AJITOA RASMI KIKOSI CHA CHAN, AENDA AFRIKA KUSINI KUANZA MAISHA MAPYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda hatajiunga kabisa na kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mchezo dhidi ya Rwanda Jumamosi, kwa sababu kesho anakwenda Afrika Kusini kujiunga rasmi na klabu yake mpya, Baroka FC.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Banda amesema kwamba pamoja na kutopewa barua ya kuruhusiwa kuondoka na Simba kufuatia kumaliza mkataba wake, lakini anakwenda Afrika Kusini kwanza.
  Banda amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Baroka ya Ligi Kuu wiki iliyopita baada ya kung’ara katika michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini akiiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu.
  Abdi Banda (kushoto) atakosekana Taifa Stars ikimenyana na Rwanda Jumamosi kwa sababu kesho anakwenda Afrika Kusini kujiunga rasmi na Baroka FC

  “Ninakwenda Afrika Kusini kesho nikiwa na nakala yangu ya mkataba uliomalizika na Simba, nadhani kupitia nakala hii klabu yangu mpya itajua cha kufanya ili kuhakikisha taratibu za uhamisho wangu zinakamilika,”amesema Banda.
  Banda alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza michuano ya COSAFA Castle na kutwaa Medali ya Shaba baada ya ushindi wa penalti 4-2 Ijumaa dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, tena akipiga moja ya matuta hayo manne.
  Lakini beki huyo anayeweza kucheza nafasi za kiungo pia amesikitika hataichezea Taifa Stars Jumamosi katika mchezo wa kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
  “Niseme tu ninawatakia kila la heri wachezaji wenzangu waliopo na timu Mwanza waweze kuifunga Rwanda na hatimaye kuitoa kabisa katika hatua hii baada ya mchezo wa marudiano ili wasonge mbele. Naamini timu ipo vizuri kwa sasa na tutashinda,”amesema Banda aliyeichezea Simba kwa miaka miwili baada ya kujiunga nayo kutoka Coastal Union ya Tanga.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BANDA AJITOA RASMI KIKOSI CHA CHAN, AENDA AFRIKA KUSINI KUANZA MAISHA MAPYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top