• HABARI MPYA

    Wednesday, July 12, 2017

    AZAM FC WAENDA NYANDA ZA JUU KUSINI KWA MECHI ZA KIRAFIKI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inaendelea kujiweka sawa kuelekea msimu ujao, habari njema ni kuwa imealikwa kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Iringa na Njombe) kucheza mechi tatu za kirafiki.
    Azam FC inakwenda huko baada ya kupewa mwaliko maalumu na timu ya Mbeya City ya jijini Mbeya, ambayo itacheza nayo mchezo maalumu wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Sokoine Julai 22 mwaka huu.
    Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itaelekea mkoani Njombe kukipiga na timu iliyopanda msimu huu, Njombe Mji katika mtanange utakaofanyika Uwanja wa Amani Makambako mjini humo Julai 24.
    Kocha Msaidizi wa Azam FC, Iddi Nassor 'Cheche' yuko tayari kwa ziara ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania baada ya kurejea kutoka Rwanda 

    Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, watamaliza ziara hiyo kwa kuelekea mkoani Iringa kukipiga na timu nyingine iliyopanda daraja, Lipuli mchezo utakaopigwa ndani ya Uwanja wa Samora Julai 26.
    Kwa mujibu wa Meneja wa timu, Phillip Alando, kikosi cha Azam FC kitarejea jijini Dar es Salaam Julai 26 mwaka huu na kupata mapumziko ya siku mbili kabla ya kurejea mazoezini Julai 30 mwaka huu.
    Mara baada ya kufanya mazoezi kwa siku kadhaa, kikosi hicho kitacheza mechi mbili za kirafiki zitakazopangiwa tarehe baadaye ambazo ni dhidi ya Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting, zote zikifanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC WAENDA NYANDA ZA JUU KUSINI KWA MECHI ZA KIRAFIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top