• HABARI MPYA

    Saturday, May 04, 2013

    SAMATTA NA ULIMWENGU KATIKA MTIHANI MGUMU AFRIKA KESHO DHIDI YA AKINA MBESUMA

    Wawakilishi wetu Ligi ya Mabingwa; Samatta na Ulimwengu wataibeba Mazembe kesho?

    Na Prince Akbar
    TIMU ya Tanzania, Simba SC imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kama nchi bado tunawakilishwa. 
    Tanzania inawakilishwa na washambuliaji wake wawili, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu katika Ligi ya Mabingwa kupitia klabu ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
    Mabingwa hao mara nne Afrika, kesho watakuwa wenyeji wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa TP Mazembe, katika mchezo wa Marudiano Raundi ya Tatu, wakihitaji kushinda si chini ya mabao 2-0 ili kusonga mbele, baada ya awali kufungwa 3-1 ugenini.
    Mbele ya Mazembe, tena kwenye Uwanja wa nyumbani, ushindi wa 2-0 au zaidi hilo ni jambo linalowezekana.
    Katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, Mzambia Collins Mbesuma alifunga mabao mawili mjini Johannesburg na lingine likifungwa na Mnigeria Onyekachi Okonkwo, wakati la kufutia machozi la Mazembe lilifungwa na Patou Kabangu.
    Siku hiyo, Samatta alikosa bao la wazi dakika ya saba baada ya kupiga kichwa kilichopaa juu ya lango sentimita chache, lakini hakuna hakika kama Poppa au Sama Goal atawakosa Pirates leo Lubumbashi.
    Mechi nyingine za leo Ligi ya Mabingwa ni kati ya Esperance na JSM Bejaia, SM Bamako na Cotonsport, Kedus Giorgis na Zamalek, Sewe Sport na FUS Rabat, Recreativo do Libolo na Enugu Rangers, ES Setif na AC Leopards na Al Ahly dhidi ya Bizertin. 
    Kila la heri Samatta na Ulimwengu wetu, kila la heri Mazembe- mafanikio yao ni mafanikio ya Watanzania pia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SAMATTA NA ULIMWENGU KATIKA MTIHANI MGUMU AFRIKA KESHO DHIDI YA AKINA MBESUMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top