• HABARI MPYA

  Alhamisi, Mei 24, 2012

  MAKALLA AWAKABIDHI BENDERA TWIGA STARS, WAPAA ADDIS


  Twiga Stars

  TIMU ya taifa ya soka ya miguu kwa wanawake Tanzania, Twiga Stars inayotarajia kuondoka leo saa 11.05 jioni kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwenda Ethiopia imekabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.
  Twiga Stars yenye msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya mchujo kwa ajili ya Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu Equatorial Guinea.
  Mechi hiyo itafanyika Mei 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Addis Ababa wakati ile ya marudiano itachezwa Juni 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepeta tiketi ya kwenda Equatorial Guinea.
  Wachezaji walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.
  Kwa upande wa Benchi la Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi), Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na Christina Luambano (Daktari wa Timu).
  Twiga Stars ambayo msafara wake unaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu saa 6 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
  Wakati huo huo: Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa sasa itaanza Mei 27 mwaka huu badala ya Mei 26 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali. Uamuzi wa kusogeza mbele kwa siku kuanza kwa ligi hiyo uliofanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 23 mwaka huu).
  Timu 23 zitachuana katika kinyang’anyiro hicho kitakachofanyika katika vituo vya Kigoma (Uwanja wa Lake Tanganyika), Musoma (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume) na Mtwara (Uwanja wa Umoja) ambapo kinatarajia kumalizika Juni 13 mwaka huu.
  Kituo cha Kigoma kina timu za Aston Villa ya Singida, Bandari (Kagera), CDA (Dodoma), JKT Kanembwa (Kigoma), Majimaji (Tabora), Mwadui (Shinyanga) na Pamba (Mwanza).
  Ashanti United ya Ilala, Flamingo (Arusha), Forest (Kilimanjaro), Korogwe United (Tanga), Nangwa VTC (Manyara), Polisi (Mara), Red Coast (Kinondoni) na Tessema ya Temeke ziko kituo cha Musoma.
  Kituo cha Mtwara kina timu za Kurugenzi ya Iringa, Lindi SC (Lindi), Mighty Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Mpanda Stars (Rukwa), Ndanda (Mtwara), Super Star (Pwani) na Tenende (Mbeya).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAKALLA AWAKABIDHI BENDERA TWIGA STARS, WAPAA ADDIS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top