• HABARI MPYA

  Thursday, May 24, 2012

  MENEJA KILIMANJAREO ABAINI SIMBA NA YANGA ZA TANO DUNIANI, MUZIKI WETU UNAUZA ZAIDI NJE


  Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Geroge Kavishe akizungumza na Waandishi wa Habari leo wakati akitambulisha kampeni ya 100% tz Flava leo katika hoteli ya New Africa.
  UCHUNGUZI uliofanywa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe umemuonyeaha mambo mawili makubwa kuhusu Tanzania- kwanza ni muziki wa nchini kuwa bidhaa inayonunuliwa zaidi nje na pili Simba na Yanga kuwa kwenye tano ya wapinzani wa jadi jadi dunaini.
  Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya 100% TZ Flava, iliyofanyika kwenye hoteli ya New Africa mchana huu mjini Dar es Salaam, Kavishe alisema kwamba mbali na Simba na Yanga kuwa kwenye tano bora ya wapinzani wa jadi duniani, pia zinashika nafasi ya pili Afrika.   
  Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Executive Solutions, waratibu wa kampeni ya 100% tz Flava akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya New Afrika leo  
  Akiizungumzia kampeni hiyo, Kavishe alisema kwamba itatembea kwa miezi sita na itapambwa na mambo mengi mazuri ya kujivunia kuhusu Tanzania.
  Alisema kampeni hiyo itakuwa na sehemu tatu, ambayo ni kwanza kuzindua alama ya kampeni hiyo, 100% tz Flava- tusherehekee kilicho chetu.
  “Kwenye hii kampeni, imetengenezwa ili kumpa mteja raha, lakini lazima iache ujumbe, ambao ni furahia kilicho chetu.  Kampeni inahusu muziki wetu, tumetumia picha za wanamuziki wetu,”alisema Kavishe na kuongeza;
  “Kwanza nataka niwaambie kama mlikuwa hamjui, bidhaa ambayo inauzika nje zaidi kwa sasa hapa Tanzania, ni muziki wetu, watu wa nje ya nchi wananunua sana muziki wetu na ndio bidhaa inayoongoza kuuzika nje ya nchi,”alisema.
  Alisema pia wametumia picha za Simba na Yanga, klabu ambazo zinadhaminiwa na bia hiyo. “Hakuna nchi duniani, klabu zake za ndani zina ukubwa na uzito ambao Simba na Yanga zinao. Mvuto wa Simba na Yanga duniani ni wa tano kwa ukubwa. Na kwa Afrika wa pili,”alisema Kavishe.
  Aidha, Kavishe pia alisema katika kampeni hizo, pia wametumia lugha za mtaani, ambazo pia ni fahari ya Tanzania kwa mfano piga tarumbeta, neno linalowakilisha kunywa bia kwa kutumia chupa moja kwa moja na kula bata, yaani kula raha.  
  Mapema, Kavishe alisema kampeni hii ni mwendelezo wa kampeni ya Kili Jivunie Utanzania, ambayo amesema kwa kiasi kikubwa imefanikiwa.
  “Bia ya Kilimanjaro Lager ipo tangu mwaka 1954. Ilipotea wakati wa harakati za uhuru  na ikarudi mwaka 1966 kama Kilimanjaro Premium Lager na hadi leo tunasukumana nayo, tunabadilisha nembo na kadhalika, lakini bado tupo nayo,”alisema.
  Kavishe alisema bia kama maisha ya mwanadamu, inazaliwa, inakuwa, inakomaa na inakufa- lakini kudumu kwa bidhaa sokoni kunatokana na kampeni inayofanywa kuibakiza sokoni.
  Alisema uchunguzi walioufanya mwaka 2009 ili kutambua kwa nini bia ya Kilimanjaro ipo sokoni na wateja wanaionaje, uliwaonyesha kwamba bia hiyo inakubalika mno mbele ya Watanzania.
  Waandishi wakisikiliza kwa makini
  “Sisi tulikuwa tunajua ni Safari Lager, tukataka kujua bia ipi inakubalika zaidi kama ya Kitanzania, majibu yaliyokuja hatukukubaliana nayo. Hatukuamini, walisema ni Kilimanjaro Premium Lager,” alisema.
  Kavishe alisema Safari Lager iko sokoni tangu mwaka 1977 na ilikuwa inachukuliwa kama ni bia ambayo asili yake ni Tanzania kutokana na alama ya kanyumba ka msonge, lakini wateja wao wakasema ni Kilimanjaro kwa sababu ya alama ya mlima Kilimanjaro, mnyama Twiga na kufanya vitu ambavyo vinawagusa Watanzania moja kwa moja.


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MENEJA KILIMANJAREO ABAINI SIMBA NA YANGA ZA TANO DUNIANI, MUZIKI WETU UNAUZA ZAIDI NJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top