• HABARI MPYA

  Ijumaa, Mei 25, 2012

  ALAN SHEARER AMBAYE BADO HAJATOKEA KAMA YEYE ENGLAND


  Shearer wa sasa

  WAKATI michuano ya Euro 2012 iko njiani, ikiwa inaanza mwezi ujao- wapo baadhi ya magwiji waliong'ara kwenye fainali zilizopita za michuano hiyo na kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu za kudumu.
  Mmojawao ni Alan Shearer Alan aliyezaliwa Agosti 13, 1970, ambaye amecheza soka katika ngazi ya juu katika ligi ya England kwa klabu tofauti ambazo ni Southampton, Blackburn Rovers, Newcastle United na pia timu ya taifa ya England.
  Shearer enzi zake na jezi ya Three Lions
  Anatambulika kama mshambuliaji bora wa England akiwa pia mfungaji bora anayeshikilia rekodi katika klabu ya Newcastle na Ligi Kuu England. Baada ya kustaafu mpira, Shearer sasa anafanya kazi kama mchambuzi wa soka katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Wakati anakaribia kustaafu uchezaji soka, Shearer alijitahidi kupata leseni ya ukocha inayotambulika kama UEFA Pro License, na kueleza nia yake ya kuwa meneja. Mwaka 2009, aliacha kwa muda jukumu lake BBC ili kuwa meneja wa timu ya Newcastle United katika mechi zake nane za mwisho wa msimu wa 2008–09 lakini akashindwa kuiepusha isishuke daraja.
  Akiwa mzaliwa wa Newcastle, Shearer alianza kucheza soka la kulipwa mwaka 1988 katika klabu ya Southampton ambapo katika mchezo wake wa kwanza alifunga mabao matatu maarufu kama hat-trick. Alijijengea heshima kwa uchezaji wake ambao ulikuwa unatumia nguvu na uwezo wa kufunga mabao ambapo ilimwezesha kuitwa timu ya taifa pamoja na kuhamia timu ya Blackburn Rovers mwaka 1992. Shearer alikuwa mchezaji muhimu katika timu ya taifa ya England na mabao yake 34 yaliiwezesha Blackburn kushinda taji la Ligi Kuu England msimu wa 1994–95. Alichaguliwa Mchezaji Bora na Chama cha Waandishi England mwaka 1994 na akashinda tuzo ya Mchezaji Bora mwaka 1995. Msimu wa 1995–96, ulishuhudia Shearer akicheza kwa mara ya kwanza Ligi ya Mabingwa na kumaliza mfungaji bora wa Ligi Kuu na mabao 31. Pia alikuwa mfungaji bora katika Kombe la Ulaya 1996 akiwa na timu ya taifa ya England, ambapo alifunga mabao matano, na akawa mfungaji wa Ligi Kuu England msimu 1996–97 akifunga mabao 25.
  Baadaye alihamia katika timu aliyokuwa anaipenda tangu utotoni ya Newcastle United baada ya mafanikio ya Euro ’96 kwa kitita kilichovunja rekodi wakati huo cha paundi milioni 15 ambapo aliichezea timu hiyo hadi anastaafu. Ingawa alishindwa kupata mafanikio kama aliyokuwa nayo Blackburn Rovers, Shearer alipata tuzo ya mshindi wa pili katika Ligi Kuu na Kombe la FA, na tuzo yake ya pili ya Mchezaji Bora Ligi Kuu. Baada ya kuchaguliwa nahodha wa timu taifa ya England mwaka 1996 na nahodha wa Newcastle mwaka 1999, alistaafu soka la kimataifa baada ya Euro 2000, ambapo alicheza mechi 63 na kufunga mabao 30 kwa timu nchi yake.
  Shearer alizaliwa Gosforth, Newcastle mwaka wa 1970 ambapo wazazi wake Alan na Anne Shearer walikuwa wachapakazi. Shearer alishauriwa na baba yake kucheza mpira akiwa na umri mdogo nay eye aliendelea hata akiwa shule. Alisoma katika shule ya Gosforth Central Middle na Gosforth High School. Wakati anakuwa kisoka, alipenda kucheza nafasi ya kiungo kwasababu aliona ndiyo inayomfanya aonekane kucheza.
  Shearer alikuwa nahodha wa timu yake ya shule na pia kuisaidia timu ya Newcastle City Schools kushinda taji ya wachezaji saba kila upande katika mashindano yaliyofanyika St James' Park. Badaye alijiunga na Wallsend Boys Club akiwa chipukizi. Wakati anaichezea timu hii, alionekana na skauti kutoka Southampton anayejulikana kama Jack Hixon, ambapo Shearer alikuwa nafanya mazoezi na timu yao ya vijana wakati wa majira ya joto. Shearer alifuzu majaribio katika klabu za daraja la kwanza ambazo ni West Bromwich Albion, Manchester City na Newcastle United, kabla ya kupewa mkataba ya vijana na timu ya Southampton, April mwaka 1986.
  Baada ya msimu miwili akiwa na timu ya vijana, Shearer alipandishwa hadi kuchezea timu ya kwanza. Mechi yake ya kwanza akiwa mchezaji wa Southampton ilikuwa Machi 26, 1988 akiingia kama mchezaji wa akiba katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Chelsea.
  Wiki mbili baadaye, alikuwa katika kikosi cha kwanza katika mechi dhidi ya Arsenal na kufunga hat-trick katika ushindi wa mabao 4-2 na hivyo basi kuvunja rekodi ya miaka 30 iliyowekwa na Jimmy Greaves ya mchezaji chipukizi kufunga hat-trick katika ligi ya juu. Wakati anafunga hat-trick, Shearer alikuwa na miaka 17 na siku 240. Shearer alimaliza msimu wa 1987–88 na mabo matatu katika michezo mitano na kuzawadiwa mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa.
  Kutoka Southampton, Shearer alihamia Blackburn Rovers ambapo aliichezwea kuanzia mwaka 1992 hadi 1996. Ingawa bosi wa Manchester United, Alex Ferguson, alimtaka Shearer, alizidiwa kete, ujanja na fedha za mdhamini wa Blackburn, Jack Walker, aliyemg'oa mshambuliaji huyo kutoka Saints hadi Ewood Park katika majira ya joto ya 1992.
  Msimu wake wa kwanza ulikuwa wa maajabu kwani alikosa nusu ya msimu huo kutokana na kuwa majeruhi wakati wa mechi dhidi ya Leeds, lakini alifunga mabao 16 katika michezo 21 alizocheza. Shearer pia alikuwa mchezaaji wa kutegemewa katika timu ya taifa ya England msimu huo kwani alifunga bao lake la pili la kimataifa katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 1994 wakati wa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Uturuki.
  Shearer baadaye alihamia timu ya Newcastle United kuanzia 1996 hadi 2006 alipostaafu soka. Baada ya Euro 96, Manchester United kwa mara nyingine tena waliitafuta kwa udi na uvumba saini ya Shearer. Mshambuliaji huyo anakiri kuwa nusura ajiunge na Mashetani Wekundu baada ya mazungumzo marefu na meneja wa Man United, Alex Ferguson. Hata hivyo, mmliki wa Blackburn Rovers, Jack Walker, aligoma kumuuza Shearer. Baadaye Manchester United pamoja na Newcastle United walikubaliana ada ya uhamisho na Blackburn Rovers, ambapo Shearer alikuwa tayari kujiunga na Manchester United lakini katika dakika ya mwisho Kevin Keegan aliomba kukutana na Shearer na kumshawishi kuwa maisha yake yapo St. James Park. Julai 30 mwaka 1996, Shearer alijiunga na timu yake ya utotoni ambayo ilikuwa ikifundishwa na mtu aliyekuwa anamhusudu; Kevin Keegan.
  Shearer alichezea mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya Newcastle Agosti 17, 1996 dhidi ya Everton, na kuendeleza utikisaji wake wa nyavu ambapo alimaliza mfungaji bora wa Ligi Kuu England kwa msimu wa tatu mfululizo. Hata hivyo taji la Ligi Kuu England ilikuwa taabu kwa Newcastle kupata ambapo walimaliza katika nafasi ya pili mfululizo na kupelekea Keegan kubwaga manyanga.
  Tangu amestaafu soka, wametokea washambuliaji wengi England, wakiwemo wa sasa akina Wayne Rooney, lakini bado inaaminika hajatokea wa kufikia makali ya mkali huyu wa mabao. Labda tusubiri siku zijazo, atatokea wa kumpiku Shearer, ila kwa sasa bado.
  Shearer wa Newcastle

  WASIFU WAKE:
  JINA: Alan Shearer Alan
  KUZALIWA: 13 Agosti 1970 (Miaka 40)
  ALIPOZALIWA: Gosforth, Newcastle, England
  KLABU ALIZOCHEZEA:
  Mwaka    Klabu
  1988–1992 Southampton (Mechi 118, mabao 23)
  1992–1996 Blackburn Rovers (Mechi 138, mabao 112)
  1996–2006 Newcastle United (Mechi 303, mabao 148)
  (Tangu 1992 hadi 2000, ameichezea England mechi 63, ameifungia mabao 30)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ALAN SHEARER AMBAYE BADO HAJATOKEA KAMA YEYE ENGLAND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top