• HABARI MPYA

  Jumatano, Mei 23, 2012

  HAWA ISMAIL AWANOA MISS KIGAMBONI 2012

  MAZOEZI kwa ajili ya kushiriki shindano la  kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni mwaka huu 'Miss Kigamboni City 2012' yameshaanza mapema wiki hii imefahamika.
  Shindano hilo limepangwa kufanyika ifikapo Juni 15 kwenye ukumbi wa Navy Beach ulioko huko Kigamboni hapa jijini Dar es Salaam.
  Akizungumza jana jijini, Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa maandalizi ya kinyang'anyiro hicho yanaendelea na warembo tayari wameshaanza mazoezi kwenye ukumbi wa Break Point ulioko Posta jirani na Club Billicanas.
  Alisema kuwa bado milango iko wazi kwa warembo wenye sifa kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini wanakaribishwa kushiriki kuwania taji hilo.
  Aliongeza kuwa kampuni yake imejipanga kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa bora na kuwapata washiriki watakaokwenda kutwaa taji la Kanda ya Temeke na hatimaye taji la taifa la Redd's Miss Tanzania baadaye mwaka huu.
  "Kila kitu ni maandalizi, tumejiandaa katika kufanya mchakato wa kupata warembo wenye sifa ili waweze kwenda kuiwakilisha vyema Kigamboni katika mashindano ya Kanda," alisema Somoe.
  Aliwataja warembo ambao wameshaanza mazoezi kuwa ni pamoja na Caroline Peter, Theopisther Wenso, Sophia Martime, Amina Aboubakar, Aisha Rajab, Rosemary Peter, Mariam Mbulilo, Julieth Phili na Doreen Kweka.
  Warembo hao wanafanya mazoezi chini ya Hawa Ismail (pichani) ambaye alikuwa mshindi ya shindano la Kanda ya Temeke mwaka 2003.
  "Bado tunakaribisha wadau wa sanaa ya urembo kutudhamini shindano hili, tunaamini uwepo wao ndio utafanikisha ubora na hadhi ya shindano letu mwaka huu kama tulivyodhamiria," aliongeza.
  Aliwataja wadhamini ambao tayari wamethibitisha kudhamini shindano hilo ni pamoja na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's, Dodoma Wine na NSSF.
  Taji la taifa la shindano hilo linashikiliwa na Salha Israel ambaye alitokea katika Kanda ya Ilala.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HAWA ISMAIL AWANOA MISS KIGAMBONI 2012 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top